Skip to content
BoT yapongeza mafanikio ya Mpango wa Makazi

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amepongeza Taasisi ya Watumishi Housing Investiment (WHI) kwa kazi nzuri wanayofanya katika kutekeleza mpango wa makazi kwa watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii.     

Gavana Tutuba alitoa pongezi hizo alipokutana na Afisa Mtendaji Mkuu wa WHI, Dkt. Fred Msemwa, katika Ofisi za Benki Kuu jijini Dar es Salaam na kujadiliana masuala mbalimbali kuhusu uendeshaji wa Taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2014.

Gavana alisema kuwa BoT inatambua na kuthamini mchango wa WHI katika kuboresha sekta ya nyumba nchini na kuinua uchumi wa wananchi. Alisema kuwa BoT kama msimamizi wa sekta ya fedha itaendelea kushirikiana na WHI ili kuiwezesha Taasisi hiyo kufikia malengo na mipango iliyojiwekea.

Aidha, Gavana alitoa wito kwa taasisi hiyo kubuni mikopo mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya wateja pamoja na kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha ili kuwezesha upatikanaji wa nyumba bora kwa watumishi wa umma.

Kwa upande wake, Dkt. Msemwa alisema kuwa WHI inajivunia kuwa taasisi inayotekeleza mpango wa makazi kwa watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ufanisi na ubora.

Alisema kuwa WHI inaendelea kujenga nyumba za gharama nafuu katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutumia teknolojia ya kisasa ambapo mpaka sasa wamefanikiwa kujenga nyumba 983.  

Dkt. Msemwa aliongeza kuwa WHI inaendelea kutoa elimu na kuhamasisha watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kuhusu faida za kujiunga na mifuko ya uwekezaji inayosimamiwa na taasisi hiyo.

Alisema kuwa WHI inaamini kuwa kwa kushirikiana na BoT na wadau wengine, itaweza kufikia malengo yake ya kutoa huduma bora za nyumba kwa watumishi na kuchangia katika maendeleo ya nchi.

WHI inasimamia Mifuko ya Uwekezaji ambayo ni: Mfuko wa Uwekezaji katika Milki (REIT) na Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja (CIS) ambapo kwa sasa WHI inaendesha MFUKO WA FAIDA.