BoT yaendeleza ushirikiano wa kimataifa katika mikutano ya IMF na Benki ya Dunia

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, pamoja na Naibu Gavana, Dkt. Yamungu Kayandabila, wameshiriki Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB) iliyofanyika jijini Washington D.C., Marekani kuanzia tarehe 13 hadi 18 Oktoba 2025.

Katika mikutano hiyo, Gavana Tutuba alifanya mazungumzo na viongozi wa Benki ya Viwanda na Biashara ya China (ICBC), akiwemo Mkurugenzi Mtendaji Bw. Peter Poon na Mkurugenzi wa Muundo wa Masoko ya Kimataifa Bi. Yoyo Ye. Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya BoT na ICBC, hususan katika eneo la uhifadhi wa akiba ya taifa. Viongozi hao walijadili fursa za uwekezaji kupitia ununuzi na uhifadhi wa dhahabu, hatua inayotarajiwa kuongeza akiba ya fedha za kigeni na kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha nchini Tanzania.

Aidha, Gavana Tutuba alishiriki Mkutano wa 52 wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika (Africa Group 1 Constituency Policy Dialogue), uliofanyika pembezoni mwa mikutano hiyo. Mkutano huo ulihusisha Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi 14 wanachama wa IMF, akiwemo Tanzania. Makubaliano yaliyofikiwa yalilenga kuimarisha mikakati ya kukuza uwekezaji wa sekta binafsi na kuongeza mapato ya ndani ili kukabiliana na kupungua kwa mikopo na misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo. Tanzania ilitajwa kufanya vizuri katika kuongeza uwazi wa bajeti na ukusanyaji wa mapato ya ndani, huku ikitekeleza mageuzi ya mifumo ya kodi na matumizi ya teknolojia za kidijitali.

Kwa upande wake, Dkt. Kayandabila alishiriki kikao cha Taasisi ya Usimamizi wa Uchumi na Fedha katika Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (MEFMI), kilichojadili fursa na changamoto za matumizi ya Akili Unde (AI) katika uchumi. Majadiliano yalijikita katika namna AI inavyoweza kusaidia ukusanyaji wa mapato, uchambuzi wa data kwa ajili ya maamuzi ya kisera, na usimamizi wa huduma za kifedha. Hata hivyo, changamoto kama uhaba wa wataalamu, miundombinu duni, na masuala ya usalama wa taarifa zilitambuliwa kama vikwazo vinavyohitaji kushughulikiwa.

Ushiriki wa viongozi hawa wa BoT katika mikutano hiyo ni ishara ya dhamira ya Tanzania kuendelea kushirikiana na taasisi za kimataifa katika kuimarisha uchumi wa taifa, kukuza uwazi wa bajeti, na kuongeza mapato ya ndani kupitia sera madhubuti na matumizi ya teknolojia za kisasa.