Skip to content
Orodha ya Taasisi Zinazosimamiwa na Benki Kuu

Benki Kuu ya Tanzania ina jukumu la kudhibiti na kusimamia benki zote, taasisi za fedha na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni nchini. Aidha, Benki Kuu ina jukumu la kudhibiti na kusimamia masuala yote ya fedha yanayohusu mifuko ya hifadhi ya jamii, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) nchini Tanzania.

Ufafanuzi wa Baadhi ya Istilahi Muhimu

  1. Shughuli za Kibenki: Ni shughuli za kupokea fedha kutoka kwa umma kupitia amana zinazoweza kurejeshwa zinapohitajika, baada ya kipindi maalumu au baada ya kutoa taarifa ya awali. Shughuli hizi pia zinajumuisha ukusanyaji wa fedha kupitia uuzaji au uwekaji wa mara kwa mara wa hati fungani, vyeti, hati za ahadi au dhamana nyingine, kwa lengo la kutumia fedha hizo, zote au sehemu yake, kutoa mikopo au kufanya uwekezaji kwa niaba na kwa hatari ya mhusika anayefanya shughuli hizo.
  2. Benki: Ni taasisi inayojishughulisha na utoaji wa huduma za kibenki.
  3. Taasisi ya Fedha: Ni taasisi inayofanya shughuli za kibenki, lakini yenye mipaka katika ukubwa wa shughuli zake, maeneo inayohudumia au aina ya huduma inazoruhusiwa kutoa, kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Benki Kuu au masharti ya leseni yake.
  4. Benki Inayotoa Huduma Kamili za Kibenki: Ni benki au taasisi ya fedha inayoruhusiwa kufanya shughuli zote za kibenki kwa mujibu wa masharti ya Sheria husika.
  5. Benki Inayotoa Huduma Zenye Ukomo: Ni benki au taasisi ya fedha inayofanya shughuli za kibenki kwa kiwango kilichowekewa mipaka, ikiwemo vizuizi katika kupokea amana zinazoweza kutolewa wakati wowote zinapohitajika au kupitia hundi.
  6. Benki ya Huduma Ndogo za Fedha: Ni benki au taasisi ya fedha inayotoa huduma za kibenki hasa kwa watu binafsi, vikundi na biashara ndogo na ndogo sana katika maeneo ya vijijini au mijini.
  7. Taasisi ya Huduma Ndogo za Fedha: Ni taasisi inayojishughulisha na utoaji wa mikopo midogo ya fedha ambayo inasimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania, kwa mujibu wa ufafanuzi huu.
  8. Benki ya Jamii: Ni taasisi ya fedha inayohudumia eneo maalumu la kijiografia, ambayo shughuli zake kuu zinahusisha kupokea amana, kutoa mikopo na kufanya shughuli nyingine zinazoruhusiwa na Benki Kuu ya Tanzania.