Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, ameshiriki Kikao cha 60 cha Kamati ya Magavana wa Benki Kuu (CCBG) wa nchi wanachama wa SADC, kilichofanyika Mei 16, 2025, jijini Maputo, Msumbiji.
Kikao hicho kililenga kujadili hali ya uchumi wa ukanda wa SADC, kuimarisha ushirikiano wa kikanda, na kukabiliana na changamoto mpya za kisera zinazotokana na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi duniani.
BoT iliwasilisha mada kuhusu athari za matukio ya kimataifa kwa nchi za SADC, ikigusia hatari ya kupungua kwa misaada kutoka Marekani, ushuru mpya kwa bidhaa kutoka SADC, sintofahamu kuhusu hatma ya Sheria ya Ukuaji wa Biashara Afrika (AGOA) na mgogoro unaoendelea DRC na athari zake kwa majirani.
BoT ilisisitiza haja ya ushirikiano wa karibu zaidi baina ya nchi za SADC ili kujenga uthabiti wa kiuchumi na uwezo wa pamoja kukabiliana na changamoto hizo.
Ripoti ya kamati ndogo ya uchumi ya SADC ilionesha ukuaji wa uchumi kushuka hadi asilimia 3.1 mwaka 2024. Hata hivyo, Tanzania (5.5%) na DRC (7.9%) ziliongoza kwa ukuaji wa juu. Tanzania pia ilitajwa miongoni mwa nchi chache zilizotimiza vigezo vya uchumi imara, ikiwemo mfumuko mdogo wa bei, deni la serikali linalohimilika, nakisi ndogo ya urari wa malipo, na kiwango cha chini cha mikopo kutoka Benki Kuu.
Akizungumza kuhusu mifumo ya malipo, Gavana Tutuba alisisitiza umuhimu wa kuendeleza kwa wakati mmoja mfumo wa TCIB kwa miamala midogo na SADC-RTGS kwa miamala mikubwa ya kuvuka mipaka.
Alieleza kuwa Tanzania ina mifumo bora ya malipo – TIPS kwa miamala midogo na TISS kwa mikubwa – inayoweza kuwa mfano wa kuigwa na nchi za SADC katika kuunganisha mifumo ya kifedha ya kikanda.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa wito wa nchi za SADC kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sera za fedha, mifumo ya malipo, na ufuatiliaji wa mwenendo wa uchumi wa kikanda kwa ajili ya ustawi wa pamoja.