Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amesema kuwa Tanzania itaendelea kushiriki kikamilifu na kutekeleza matakwa ya kimataifa katika kupambana na kudhibiti uhalifu wa kifedha, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kulinda usalama wa mfumo wa kifedha wa taifa.
Akizungumza leo katika ufunguzi wa mkutano kati ya Ujumbe wa Tanzania na Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Kudhibiti Fedha Haramu (FATF), uliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali inatambua ukubwa wa changamoto za uhalifu wa kifedha na imejidhatiti kuzikabili kwa kutumia viwango vya kimataifa.
“Tanzania imechukua hatua madhubuti za kuimarisha mifumo yake ya kupambana na fedha haramu. Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha uwezo wa taasisi zinazohusika kwa kuwapatia watumishi mafunzo, rasilimali na vifaa vinavyohitajika,”alisema.
Ameeleza kuwa baada ya tathmini zilizofanywa na taasisi za Kikanda na Kimataifa za Kuthibiti Uhalifu wa Kifedha mwaka 2021 na 2022, Tanzania imechukua hatua madhubuti za kuimarisha mifumo yake ya kupambana na fedha haramu. Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha uwezo wa taasisi zinazohusika kwa kuwapatia watumishi mafunzo, rasilimali na vifaa vinavyohitajika.
Amesema kuwa Serikali imeyapa kipaumbele maeneo muhimu katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kifedha, ikiwemo kufanya marekebisho ya sheria na sera, kutumia takwimu na teknolojia za kisasa, kuimarisha usimamizi katika sekta ya nyumba na ardhi, kujenga uwezo kwa wadau husika, pamoja na kuimarisha udhibiti na usimamizi wa taasisi za kifedha.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa baada ya Tanzania kupokea Mpango Kazi kutoka FATF, Serikali ilifanya maamuzi ya ngazi ya juu ya kisera na kiutendaji ili kuimarisha juhudi za kupambana na uhalifu wa kifedha nchini.
Naye, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba alisema kuwa hatua mahsusi zimechukuliwa ili kuimarisha usimamizi wa watoa huduma za mali za kidijitali na kuongeza uwazi katika sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali. Ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali na matumizi bora ya takwimu pia vinaimarishwa ili kusaidia mamlaka kugundua na kukabiliana na uhalifu wa kifedha kwa ufanisi zaidi.