Naibu Gavana Msemo: Serikali zihamasishe vyanzo mbadala vya fedha

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Sauda Msemo, amezitaka serikali za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara kuimarisha ukusanyaji wa rasilimali za ndani ili kupunguza utegemezi mkubwa kwa misaada ya kigeni inayopungua.

Akizungumza tarehe 28 Aprili 2025 katika mjadala ulioandaliwa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Uchumi wa Kanda ya Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara 2025, Bi. Msemo alisema kuna umuhimu wa kupanua wigo wa vyanzo vya fedha kwa kutafuta washirika wapya na mbinu mbadala za kupata fedha.

“Serikali zetu zinapaswa kujitahidi kuongeza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi wa misaada kutoka mataifa ya nje. Pia, tunapaswa kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili kuimarisha uwezo wetu wa kifedha,” alisema.

Bi. Msemo alielezea kuwa mabadiliko ya ghafla katika sera za misaada za Marekani, yakiwemo kuondolewa kwa misaada katika sekta muhimu kama elimu, afya na miundombinu, yameleta changamoto kubwa kwa nchi nyingi Kusini mwa Jangwa la Sahara.  

“Hatua za haraka zilizochukuliwa ni pamoja na kuongeza mgao wa bajeti kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa programu muhimu, huku bajeti za miaka ijayo zikizingatia uendelevu wa miradi katika sekta hizo muhimu,”alisema.     

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic nchini, Bw. Manzi Rwegasira, alisema ili sekta binafsi ivutie uwekezaji, ni muhimu kwa serikali kuimarisha mazingira ya biashara kwa kuboresha mifumo ya kodi, kutoa dhamana kwa mikopo na kushirikiana katika uwekezaji kwenye miradi.  

Naye, Naibu Mkurugenzi wa IMF Idara ya Afrika, Bi. Cathy Pattillo, alisema nchi nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zina uwezo wa kuongeza mapato ya ndani, lakini kiwango cha ukusanyaji kodi kwa sasa bado kiko chini ya matarajio ukilinganisha na uwezo uliopo. Alisisitiza kuwa mapato ya ndani ni chanzo cha uhakika na endelevu cha maendeleo.          

Mwakilishi wa IMF nchini, Bw. Sebastian Acevedo, amesisitiza umuhimu wa kuwa watumishi wenye ujuzi wa kutosha ili kuweza kufaidika na idadi kubwa ya watu barani Afrika ili kukabili changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazoibuka.

Kwa mujibu wa ripoti ya IMF, shughuli za kiuchumi katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ziliongezeka kwa asilimia 4.0 mwaka 2024, ikiwa ni juu kwa asilimia 0.4 kuliko makadirio ya awali. Ukuaji huo umechangiwa na uwekezaji wa umma, mauzo ya bidhaa nje, na juhudi za kuendeleza utofauti wa uchumi.

Ripoti hiyo imeonyesha pia kuwa mfumuko wa bei umepungua kwa kiasi kikubwa, ukifikia wastani wa asilimia 4.5 mnamo Februari 2025, ukilinganishwa na asilimia 6.5 mwishoni mwa mwaka 2023 na karibu asilimia 10 mwishoni mwa mwaka 2022. Hali hii imetokana na sera madhubuti za fedha pamoja na kushuka kwa bei za chakula na nishati duniani.