Benki Kuu ya Tanzania imetawazwa Mshindi wa Kwanza Kitaifa katika Kundi la Taasisi za Udhibiti, Ubora na Viwango katika Maonesho ya Wakulima - Nanenane yaliyohitimishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 8 Agosti jijini Mbeya.
Aidha, Benki Kuu imeshiriki katika Maonesho ya Nananane Zanzibar na katika Kanda zaa Kati jijini Dodoma, Kaskazini jijini Arusha, Kusini huko Lindi na Kanda ya Ziwa jijini Mwanza. Katika kanda zote, BoT imeibuka Mshindi wa kwanza katika Kundi la Mamlaka za Udhibiti na Usimamizi.
Maonesho hayo ya kimataifa yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale yalifunguliwa rasmi tarehe 01 Agosti 2023 na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ambaye pia alitembelea banda la Benki Kuu na kujionea namna wataalamu wake wanavyotoa elimu kwa wananchi.
Banda la Benki Kuu lilikuwa mojawapo ya vivutio muhimu katika maonesho hayo, na lilipokea wageni wengine mashuhuri wakiwemo Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri Mkuu Mstaafu, Bw. Mizengo Pinda, pamoja na Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge ya Bajet, na Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo. Naibu Gavana, Bw. Julian Banzi Raphael, aliongoza ujumbe wa Benki Kuu katika kushiriki maonesho hayo, na pia alikuwa mwenyeji wa wageni hao mashuhuri.
Benki Kuu ilichukua fursa ya maonesho hayo kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya kiuchumi na fedha. Elimu hiyo ilihusu utafiti na sera za uchumi, uwekezaji katika dhamana za serikali, usimamizi wa mifumo ya malipo ya taifa na sekta ya fedha.
Aidha, walijifunza kuhusu kazi za Bodi ya Bima ya Amana, mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania, utatuzi wa malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha, na utambuzi wa alama za usalama katika noti zetu.
Zaidi ya hayo, Benki Kuu ilipata maoni na ushauri muhimu kutoka kwa wadau na wananchi mbalimbali kuhusu jinsi ya kuwafikia na kuwahudumia vyema, huku ikiendelea kuboresha utendaji wake katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi.
Ushindi huu wa Benki Kuu ya Tanzania katika Maonesho ya Nanenane kitaifa na kikanda ni uthibitisho wa juhudi zake za kuchangia katika maendeleo ya nchi kwa kutoa elimu na huduma bora kwa wananchi na wadau wa sekta ya fedha.
BoT YATIKISA MAONESHO YA NANENANE KITAIFA NA KIKANDA