Skip to content
Gavana BoT azindua Mtaala wa Wakufunzi wa Elimu ya Fedha

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba leo Desemba 12, 2023 amezindua Mtaala wa Wakufunzi wa Elimu ya Fedha waliorasimishwa katika Ofisi za Makao Makuu Ndogo ya Benki Kuu jijini Dar es Salaam.

Akizindua mtaala huo, Gavana Tutuba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Huduma Jumuisha za Fedha amesema utekelezaji wa mtaala huu utasaidia kutatua changamoto zinazotokana na uhaba au upungufu wa ujuzi wa usimamizi binafsi wa masuala ya fedha

“Changamoto hizi zinaweza kusababisha uzorotaji wa ufanisi wa wafanyakazi katika taasisi za fedha tunazosimamia na kuathiri mfumo wa fedha nchini au kusababisha ongezeko la mikopo chechefu kutokana na wakopaji kutokua na umakini na ujuzi binafsi wa kusimamia masuala ya fedha”,alisema.

Aliongeza kuwa Baraza la Huduma Jumuishi za Fedha linaazimia kwamba changamoto hizo zitokomezwe nchini huku akisisitiza utekelezaji wa mtaala huu  leo utatimiza azma hiyo.

Pamoja na kutoa pongezi kutokana na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika utunzi wa mtaala huu Gavana Tutuba ameiagiza Sekretarieti ya Baraza la Huduma Jumuishi za Fedha kuhakikisha kuwa utekelezaji wa programu hii unakuwa wa uendelevu, shirikishi, wenye ubunifu, uweze kupimwa na utolewe  taarifa.

“Ningependa kuwaaagiza yafuatayo, kuhakisha wananchi wengi walio nje ya mashule na vyuo wanafikiwa na elimu na ujuzi huu, ushirikishwaji wa wadau wengi ilikupata maoni, mawazo na mbinu za kuwafikia wengi, ubunifu na teknoligia katika kutoa elimu, kupanga na kutekeleza mikakati ya kuhakikisha inapima ufanisi wake na utoaji wa taarifa mbalimbali kwa wananchi na  uongozi kwa ajili ya usimamizi mzuri”.

Awali, Naibu Gavana Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, alisema mtaala huo una lengo la kukuza maadili katika matumizi ya fedha.

Pia, aliongeza kuwa uzinduzi wa mtaala huu ni kielezo cha jitihada zinazoendelea kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya fedha kutokana na umuhimu wake katika ustawi wa uchumi wa nchi.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, Beng’i Isaa amesema kutokua na elimu ya masuala ya fedha kunapelekea wananchi hususani wanawake kufanya maamuzi yasiyo na tija ikiwemo kuchukua mikopo ‘kausha damu’ bila kujua hasara zake.

“Wanawake wengi wamekuwa wakikopa hususani hii mikopo ya kausha damu bila kufahamu masuala ya riba.

“Sasa wakati wa kufanya marejesho ndipo wanapogundua hilo, iwapo wangekuwa na elimu ya fedha changamoto hizi zisingekuwepo” alisema

Aliongeza kuwa utekelezaji wa mtaala huo utasaidia watu kupata ujuzi wa kuzitawala fedha na sio fedha kuwatawala watu.

Kwa upande wake Prof. Andrew Mbwambo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Iringa, ambacho ni miongoni mwa vyuo vyilivyoingia makubaliano na BoT katika kutoa elimu hiyo, ameipongeza Benki Kuu kwa kushirikisha vyuo vya serikali na vyuo binafsi katika maandalizi ya mtaala huo.