Skip to content
Ujumbe wa Benki Kuu ya Somaliland Wazuru BoT kujifunza Mifumo ya Fedha

Katika jitihada za kuimarisha mifumo yake ya fedha, ujumbe kutoka Benki Kuu ya Somaliland umefanya ziara Benki ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam tarehe 4 Desemba, 2023.

Ujumbe huo umeshiriki katika majadiliano na viongozi wa BoT yaliyolenga kuimarisha miundombinu yao ya fedha kupitia uchunguzi wa kina wa mifumo imara ya Tanzania.

Moja ya mambo muhimu ya ziara hii ilikuwa ni kumtembelea Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania anayehusika na Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi Sauda Kassim Msemo. Mazungumzo na ujumbe huo yalijikita katika nyanja mbalimbali zikiwemo mifumo ya malipo, usimamizi wa sekta ya fedha, ustawi na huduma jumuishi za fedha, na mifumo ya kisheria.

Kurugenzi ya Mifumo ya Taifa ya Malipo ilitoa maelezo kwa kina kuhusu mifumo ya malipo Tanzania. Majadiliano yalijikita katika sheria, kanuni, sekula na miongozo katika usimamizi wa mifumo ya malipo. Maelezo maalum yalitolewa kuhusu mfumo ya malipo kwa njia ya hundi - TACH, mfumo wa utumaji wa fedha kieletroniki – EFT, mfumo unaotumika kutuma na kupokea malipo kati ya benki za biashara na kati ya benki hizo na Benki Kuu –TISS, na Mfumo wa Malipo ya Papo kwa Hapo Tanzania - TIPS.

Pia, Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha iliangazia mikakati iliyotumika nchini Tanzania kuimarisha huduma jumuishi za fedha. Ujumbe huo kutoka Benki Kuu ya Somaliland ulipata ufahamu juu ya athari za kanuni mbalimbali kwenye sekta ya fedha na juhudi zilizofanywa kuhakikisha uwepo wa mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza huduma jumuishi za fedha.

Wakati wa majadiliano, Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha ilisisitiza jukumu muhimu la kusimamia benki katika kuhakikisha utulivu na uadilifu wa taasisi za fedha. Mkazo uliwekwa kwenye umuhimu wa taasisi za fedha kufuata sheria na kanuni zilizopo, huku kukiwa na msisitizo kuhusu jukumu la Benki Kuu kama mdhibiti katika kusaidia ukuaji wa mfumo wa Huduma za Fedha za Kidijitali (DFS). Sababu za mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika jitihada hii pia zilijadiliwa, na kutoa maarifa muhimu kwa ujumbe wa Somaliland.

Ziara hiyo ilikuwa fursa muhimu kwa ujumbe wa Benki Kuu ya Somaliland kubadilishana maarifa na mazoea bora na wenzao wa Tanzania, na ku
angalia maeneo ya ushirikiano. Ujumbe ulionyesha shukrani zao kwa Benki Kuu ya Tanzania kwa kuratibu vizuri ziara hiyo, na kuwa na matumaini ya kutumia mambo waliyojifunza kuimarisha maendeleo na uthabiti wa sekta ya fedha nchini mwao.