Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kuimarisha juhudi za kuunganisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika usimamizi wa sekta ya fedha, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uwekezaji endelevu na kuongeza upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko hayo.
Juhudi hizo zimebainishwa katika Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), unaofanyika jijini Antalya, Uturuki, ambapo Benki Kuu kwa kushirikiana na Mtandao wa Benki Kuu na Mamlaka za Usimamizi wa Sekta ya Fedha kwa ajili ya Kuhamasisha Mfumo wa Fedha Rafiki kwa Mazingira (NGFS), iliandaa mijadala miwili iliyofanyika tarehe 12 na 13 Novemba 2026 katika Banda la Maonesho la Tanzania.
Mijadala hiyo ilijikita katika nafasi ya sekta ya fedha katika kuimarisha ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, kuboresha usimamizi wa vihatarishi vinavyotokana na mabadiliko hayo na kuongeza upatikanaji wa fedha za tabianchi, hususan kwa nchi zinazoendelea.
Akifungua mjadala wa kwanza kuhusu kuimarisha ustahimilivu wa sekta ya fedha, Meneja wa Idara ya Uthabiti wa Sekta ya Fedha wa Benki Kuu, Bi. Edista Njau, alisema mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa vihatarishi vikubwa vinavyoathiri utulivu wa uchumi na sekta ya fedha duniani.
Alieleza kuwa athari za matukio makubwa ya hali ya hewa pamoja na mabadiliko ya sera na masoko yanayotokana na jitihada za kukabiliana na tabianchi zinaongeza changamoto kwa taasisi za fedha. Hali hiyo ni muhimu zaidi kwa nchi kama Tanzania, ambazo uchumi wake unategemea kwa kiasi kikubwa sekta nyeti kwa tabianchi, ikiwemo kilimo.
Bi. Njau alibainisha kuwa Benki Kuu imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha usimamizi wa vihatarishi vya kifedha vinavyohusiana na tabianchi, ikiwemo kutoa miongozo ya usimamizi na utoaji wa taarifa kuhusu vihatarishi hivyo, kuhimiza taasisi za fedha kufanya tathmini za athari za tabianchi na majaribio ya uwezo wa kuhimili mishtuko inayotokana na mabadiliko hayo (Climate Stress Testing).
Aliongeza kuwa Benki Kuu inaendelea kushiriki katika majukwaa mbalimbali ya kitaifa yanayoratibu ajenda ya mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo Jukwaa la Uthabiti wa Sekta ya Fedha Tanzania (Tanzania Financial Stability Forum – TFSF), linaloongozwa na Gavana wa Benki Kuu.
Kwa upande wake, Mchambuzi na Mtaalamu wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Uendelevu wa Benki Kuu, Bw. Joseph Kenene, alieleza hatua zinazochukuliwa na Benki katika kuimarisha uwezo wa sekta ya fedha kukabiliana na vihatarishi vya tabianchi, ikiwemo kuanzisha Kanzidata ya Tabianchi (Climate Data Repository).
Alisema kanzidata hiyo inalenga kuunganisha taarifa za kifedha na takwimu za mazingira ili kuwezesha tathmini sahihi ya vihatarishi vya tabianchi na kusaidia taasisi za fedha kufanya maamuzi sahihi katika utoaji wa mikopo.
Naye Katibu Mkuu wa NGFS, Bw. Yann Marin, aliipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa hatua inazochukua katika kuimarisha usimamizi wa vihatarishi vya tabianchi. Alisisitiza umuhimu wa kubadilishana uzoefu, kujenga uwezo wa kitaasisi na kutumia uchambuzi wa hali mbalimbali za tabianchi katika kutathmini vihatarishi vya kifedha.
Katika mjadala wa pili uliofanyika tarehe 13 Novemba 2026, uliohusu kupunguza pengo la ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha upatikanaji wa fedha hizo kwa usawa, Meneja Msaidizi wa Idara ya Uthabiti wa Sekta ya Fedha, Dkt. Method Simbachawene, alisisitiza umuhimu wa kurahisisha masharti ya upatikanaji wa fedha kutoka taasisi za kimataifa na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kufadhili miradi ya tabianchi.
Alieleza kuwa mifumo bunifu ya ufadhili, ikiwemo mikopo yenye masharti nafuu, dhamana za mikopo na hati fungani za kijani, inaweza kusaidia kupunguza vihatarishi vya uwekezaji na kuvutia mitaji katika miradi inayolenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuelekeza fedha hizo katika sekta muhimu kama kilimo, maji na miundombinu himilivu, huku kuhakikisha wakulima wadogo, wanawake, vijana na biashara ndogo na za kati wanapata manufaa ya fursa hizo.
Mbali na mijadala hiyo, Benki Kuu ilishiriki pia katika mkutano ulioandaliwa na Benki Kuu ya Uturuki kwa kushirikiana na NGFS, uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa benki kuu, wakiwemo Gavana wa Benki Kuu ya Uturuki, Dkt. Fatih Karahan, na Gavana wa Benki Kuu ya Uholanzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa NGFS, Profesa Dkt. Olaf Sleijpen.
Kupitia ushiriki huo, Benki Kuu ilipata fursa za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kujenga uwezo wa kitaasisi, ikiwemo kupitia programu za mafunzo zinazotolewa na Benki Kuu ya Ujerumani (Deutsche Bundesbank). Mafunzo hayo yanatarajiwa kusaidia kuongeza utaalamu wa watumishi katika tathmini ya vihatarishi vya tabianchi, usimamizi wa taasisi za fedha na uendelezaji wa fedha za kijani.
Vilevile, ushiriki wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania katika mkutano huo unaunga mkono juhudi za kuandaa mtaala wa vihatarishi vya kifedha vinavyohusiana na tabianchi kwa watoa huduma za kifedha nchini, ili kuhakikisha mafunzo yanazingatia viwango vya kimataifa na mahitaji ya sekta ya fedha Tanzania.
Kwa ujumla, ushiriki wa Benki Kuu katika COP31 umeimarisha nafasi yake katika mijadala ya kimataifa kuhusu uhusiano kati ya mabadiliko ya tabianchi na uthabiti wa sekta ya fedha, huku ukifungua fursa za ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kuhamasisha uwekezaji endelevu unaolenga kuimarisha ustahimilivu wa uchumi na kuchochea maendeleo endelevu nchini.