Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, ametunukiwa tuzo maalum ya Magavana wa Benki Kuu waliopata Daraja A kwa mwaka 2026 na taasisi ya kimataifa ya Global Finance, kwa kutambua mchango wake katika usimamizi wa sera ya fedha, sekta ya fedha na kukuza huduma jumuishi za fedha.
Tuzo hiyo imetolewa tarehe 17 Oktoba 2026, jijini Bangkok, nchini Thailand, wakati wa mikutano ya mwaka ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia (World Bank Group)
Tuzo hiyo inaakisi hatua zilizopigwa na Benki Kuu ya Tanzania katika kusimamia uthabiti wa uchumi, kuimarisha mifumo ya kifedha na kupanua upatikanaji wa huduma rasmi za fedha kwa wananchi na wafanyabiashara, sambamba na juhudi za kuendeleza mfumo wa fedha unaochochea ukuaji wa uchumi jumuishi na endelevu.
Usimamizi wa Sera ya Fedha
Katika eneo la usimamizi wa sera ya fedha, Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kuchukua hatua zinazolenga kudumisha utulivu wa bei, kuimarisha thamani ya fedha na kuweka mazingira yanayosaidia ukuaji endelevu wa uchumi.
Miongoni mwa hatua hizo ni kuanzishwa kwa mfumo wa sera ya fedha unaotumia Riba ya Benki (Central Bank Rate – CBR), ulioanza kutumika Januari 2024. Mfumo huu umeimarisha uwazi na ufanisi katika utekelezaji wa sera ya fedha kwa kuweka kiwango kinachotoa mwongozo wa mwelekeo wa viwango vya riba katika soko la fedha.
Katika robo ya nne ya mwaka 2026, Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu iliamua kudumisha CBR katika asilimia 6.25, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusimamia hali ya uchumi na kudhibiti shinikizo la mfumuko wa bei. Katika kipindi hicho, mfumuko wa bei Tanzania Bara ulifikia asilimia 4.3 mwezi Agosti 2026, kiwango kilichoendelea kubaki ndani ya lengo la taifa la asilimia 3 hadi 5.
Mwenendo huo unaonesha mchango wa usimamizi wa sera ya fedha katika kudumisha utulivu wa uchumi, kulinda uwezo wa wananchi wa kununua bidhaa na huduma, pamoja na kuimarisha imani ya wawekezaji katika uchumi wa Tanzania.
Kuimarisha na Kuendeleza Sekta ya Fedha
Katika eneo la sekta ya fedha, Benki Kuu imeendelea kuimarisha usimamizi na udhibiti wa taasisi za fedha ili kuhakikisha zinafanya kazi kwa usalama, uwazi na ufanisi, huku zikichangia upatikanaji wa mitaji na huduma za kifedha kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.
Hatua hizo zinajumuisha kuimarisha mifumo ya udhibiti, kusimamia mwenendo wa taasisi za fedha na kuendeleza mifumo ya malipo inayowezesha miamala kufanyika kwa haraka, kwa usalama na kwa gharama zinazozingatia mahitaji ya watumiaji.
Miongoni mwa maendeleo muhimu ni kuanzishwa kwa Mfumo wa Malipo wa Papo kwa Hapo (Tanzania Instant Payment System – TIPS) ambao umekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi wa malipo ya kielektroniki na kurahisisha miamala kati ya benki na huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi.
Kwa ujumla, hatua hizi zimechangia kujenga mazingira yanayowezesha taasisi za fedha kutoa huduma kwa ufanisi zaidi, kuimarisha imani ya wananchi katika mfumo rasmi wa fedha na kuweka msingi wa ukuaji wa sekta ya fedha unaozingatia ubunifu, ushindani na uthabiti.
Kukuza Huduma Jumuishi za Fedha
Katika eneo la huduma jumuishi za fedha, Tanzania imepiga hatua katika kupanua wigo wa wananchi wanaopata na kutumia huduma rasmi za kifedha, hususan kupitia matumizi ya teknolojia za kidijitali, huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi na mitandao ya mawakala.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa FinScope Tanzania wa mwaka 2023, kiwango cha watu wazima waliokuwa na upatikanaji wa huduma rasmi za fedha kiliongezeka kutoka asilimia 86 mwaka 2017 hadi asilimia 89 mwaka 2023. Aidha, matumizi ya huduma hizo yaliongezeka kutoka asilimia 65 hadi asilimia 76 katika kipindi hicho.
Mafanikio hayo yamechangiwa na juhudi za Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali, taasisi za fedha, kampuni za mawasiliano na wadau wengine katika kupanua upatikanaji wa huduma za kibenki na mifumo ya malipo ya kidijitali. Juhudi hizo pia zinajumuisha kuratibu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa mwaka 2023–2028.
Sambamba na kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha, Benki Kuu imeendelea kusisitiza umuhimu wa elimu ya fedha ili kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi ya mapato, uwekaji wa akiba, ukopaji wenye tija, uwekezaji na matumizi salama ya huduma za kifedha. Juhudi hizi zinalenga kuhakikisha kuwa wananchi hawanufaiki tu kwa kupata huduma hizo, bali pia wanazitumia kwa ufanisi katika kuboresha maisha yao na kuimarisha ustahimilivu wao wa kifedha.
Katika kufanikisha lengo hilo, Benki Kuu imeanzisha Programu ya Waelimishaji Waliothibitishwa wa Elimu ya Fedha, inayolenga kuwafikia wananchi walio nje ya mfumo rasmi wa elimu kwa kuwapatia maarifa na ujuzi wa kusimamia fedha kwa ufanisi. Kupitia programu hiyo, waelimishaji hupatiwa mafunzo yanayozingatia mtaala maalumu ili kuwawezesha kutoa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali ya wananchi, wakiwemo wafanyabiashara, wajasiriamali na wanajamii wengine. Elimu hiyo inahusu usimamizi wa fedha binafsi, upangaji wa bajeti, uwekaji wa akiba, ukopaji wenye tija, uwekezaji na matumizi salama ya huduma za kifedha.
Vilevile, Benki Kuu kwa kushirikiana na Serikali imeendelea kuimarisha elimu ya fedha nchini kwa kuichopeka katika mitaala ya elimu rasmi. Hatua muhimu katika juhudi hizo ni kuzinduliwa kwa Mwongozo wa Kuchopeka Elimu ya Fedha katika Mitaala ya Elimu ya Juu, Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini, tarehe 2 Oktoba 2026. Mwongozo huo unalenga kuhakikisha kuwa wanafunzi katika ngazi hizo za elimu wanapata maarifa na stadi za kifedha zitakazowawezesha kusimamia fedha binafsi, kupanga bajeti, kuweka akiba, kukopa kwa uwajibikaji, kuwekeza na kutumia huduma za fedha kwa usalama na ufanisi.
Aidha, katika kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za fedha, Benki Kuu imeanzisha mfumo wa kidijitali wa SEMA NA BoT, uliozinduliwa tarehe 5 Juni 2025. Mfumo huo unawawezesha wananchi kuwasilisha malalamiko kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi za fedha, kufuatilia hatua za utatuzi na kuomba mapitio ya maamuzi pale wanapokuwa hawajaridhika. Kupitia mfumo huo, Benki Kuu inaendelea kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za fedha, huku ikitumia takwimu za malalamiko kubaini changamoto zinazowakabili watumiaji na kuhimiza maboresho katika utoaji wa huduma hizo.
Mafanikio katika maeneo hayo matatu yanaonesha mchango wa Benki Kuu katika kuimarisha misingi ya uchumi wa Tanzania na kujenga mfumo wa fedha wenye uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya ndani na nje ya nchi.
Tuzo hiyo ni heshima kwa Benki Kuu ya Tanzania na Taifa kwa ujumla, huku ikiweka msisitizo wa kuendelea kuboresha sera, mifumo ya udhibiti, ubunifu wa kifedha na elimu ya fedha ili kuhakikisha sekta ya fedha inaendelea kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi jumuishi na ustawi wa wananchi.