BoT Yaungana na Dunia Kukuza Huduma za Fedha za Kiislamu Morocco

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeungana na taasisi nyingine za kifedha duniani kushiriki katika Mkutano Mkuu wa Bodi ya Huduma za Fedha za Kiislamu (Islamic Financial Services Board - IFSB), uliofanyika katika mji mkuu wa Morocco, Rabat, kuanzia tarehe 1 hadi 4 Julai 2025.                 

Naibu Gavana, Bi. Sauda Msemo, aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo wa kimataifa, ambao unahusisha zaidi ya nchi 80 wanachama wa IFSB, wakiwemo magavana wa mabenki kuu, mawaziri wa fedha, na viongozi waandamizi kutoka taasisi mbalimbali za fedha zinazotekeleza huduma kwa mujibu wa misingi ya Sheria za Kiislamu (Shariah-compliant financial institutions).     

Katika mkutano huo, Naibu Gavana alipata fursa ya kukutana uongozi wa IFSB ukiongozwa na Katibu Mkuu, Dk. Ghiath Shabsigh, ambapo walijadiliana masuala ya kimkakati yanayohusu maendeleo ya huduma za kifedha za Kiislamu, pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusu utekelezaji bora wa mifumo ya udhibiti, uvumbuzi wa kidijitali na ushirikiano wa kimataifa katika kukuza ustawi wa sekta hiyo.   

IFSB ni taasisi ya kimataifa yenye makao yake makuu nchini Malaysia, inayojumuisha wanachama zaidi ya 190 kutoka mabenki kuu, taasisi za usimamizi wa fedha, taasisi za kifedha za Kiislamu, na mashirika ya kimataifa ya maendeleo. Lengo lake kuu ni kuweka viwango vya udhibiti na miongozo bora kwa taasisi za kifedha zinazofuata misingi ya Sharia.

Mkutano huu mkubwa wa mwaka umeendelea kuwa jukwaa muhimu kwa ajili ya kujadili mwenendo wa huduma za fedha za Kiislamu, changamoto na fursa zilizopo, huku Tanzania ikiendelea kuimarisha nafasi yake katika uwanja huo kupitia sera thabiti na ushirikiano wa kimataifa.