Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeshusha kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) kutoka asilimia 6 hadi asilimia 5.75 katika robo ya tatu ya mwaka inayoanza Julai hadi Septemba 2025.
Kiwango cha Riba cha Benki Kuu (CBR) ni kiwango kinachotumika na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika shughuli zake na benki za biashara, ambazo zinapaswa kufuata sera hiyo ndani ya wigo wa asilimia ±2.0 ya kiwango kilichowekwa.
Akizungumza katika mkutano wa viongozi w benki na waandishi wa habari, Gavana wa BoT ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema uamuzi huu unatokana na mwenendo mzuri wa kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na udhibiti wa mfumuko wa bei.
‘Uamuzi huu unaakisi imani ya Kamati katika mwenendo wa mfumuko wa bei ambao umeendelea kubaki ndani ya wigo wa asilimia 3–5. Hali hii inatokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti, kuanza kwa msimu wa mavuno, pamoja na utulivu wa thamani ya shilingi ya Tanzania”. Amesema Gavana Tutuba.
Ameongeza kuwa , Benki Kuu itatekeleza sera ya fedha ili kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki (7-day interbank rate) inabaki ndani ya wigo wa asilimia 3.75 hadi 7.75.
Kuhusu mwenendo wa uchumi wa nchi, Gavana amsema umeendelea kuimarika ukichochewa na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu na kuongezeka kwa shughuli za sekta binafsi, kutokana na kuimarika kwa mazingira ya ufanyaji biashara.
Aidha, amesisitiza kuwa hatari za misukosuko ya nje kwenye matarajio ya mwenendo wa uchumi ni ndogo, kutokana na muundo wa uchumi wa nchi ambao unategemea sekta mbalimbali za uzalishaji, pamoja na utekelezaji thabiti wa sera na programu zinazochochea ukuaji wa uchumi, ambazo zinatarajiwa kusaidia kuhimili misukosuko hiyo.
Akijibu swali la mwandishi wa habari, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki, Bw. Theobald Sabi, alisema kuwa kupungua kwa CBR kunaweza kuchangia kupunguza viwango vya riba vinavyotozwa na benki za biashara. Hata hivyo, viwango hivyo huathiriwa pia na vigezo vingine kama vile nguvu za soko na tathmini ya vihatarishi inayofanywa kwa mteja kabla ya kumpa mkopo.
Riba ya Benki Kuu kwa robo ya 4 ya mwaka 2025 itatangazwa mwezi Oktoba mwaka huu. Hii ni kulingana na kalenda ya mikutano ya Kamati ya Sera ya Fedha ya mwaka.