Serikali yasisitiza matumizi ya Shilingi katika malipo ndani ya nchi

Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa wito kwa wadau wa sekta ya utalii na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kuwa malipo ya bidhaa na huduma zote ndani ya nchi yanafanyika kwa Shilingi ya Tanzania, kama ilivyoainishwa katika Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni za Mwaka 2025.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Idara ya Uchumi wa Kimataifa na Sekta za Uzalishaji kutoka BoT, Bi. Villela Waane, katika semina ya wadau wa utalii iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, na kuongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Hassan Abbas, jijini Dodoma tarehe 28 Mei 2025.

Bi. Waane alieleza kuwa Kanuni hizo zilizochapishwa katika Gazeti la Serikali Na. 198 la tarehe 28 Machi 2025, zinatekelezwa kwa mujibu wa Kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006. Alisisitiza kuwa ni kosa la kisheria kunukuu au kutangaza bei kwa fedha za kigeni, au kupokea malipo kwa fedha hizo ndani ya nchi.

"Matumizi ya Shilingi ni muhimu kwa utekelezaji wa sera ya fedha, udhibiti wa mfumuko wa bei, na ustawi wa uchumi wa taifa. Shilingi ni ishara ya utaifa na utambulisho wetu," alisema Bi. Waane.

Naye, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha, Bw. Emmanuel Akaro, aliongeza kuwa Kanuni mpya zinaruhusu miamala michache tu kufanyika kwa fedha za kigeni. Mikataba ya malipo kwa fedha za kigeni haitaruhusiwa kuanzishwa wala kuhuishwa kuanzia tarehe 28 Machi 2025. Watalii na wageni kutoka nje ya nchi wanapaswa kubadilisha fedha kupitia benki au maduka rasmi ya kubadilisha fedha, au kutumia njia za kidigitali kama kadi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, aliwataka wadau kushirikiana na Serikali kutekeleza Kanuni hizo zenye lengo la kusaidia kuimarisha uchumi, kulinda thamani ya Shilingi ya Tanzania, na kuleta utulivu wa kifedha nchini.

Ushiriki wa BoT katika semina hiyo ni sehemu ya juhudi za kutoa elimu kwa wadau wa sekta mbalimbali nchini ili kuwaongezea uelewa kuhusu utekelezaji wa Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni za Mwaka 2025, pamoja na umuhimu wa kutumia Shilingi ya Tanzania katika miamala yote ya ndani ya nchi.