Gavana Emmanuel Tutuba, ameongoza ushiriki wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika Mikutano ya Msimu wa Kipupwe ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, iliyofanyika kuanzia tarehe 21 hadi 26 Aprili 2025, jijini Washington D.C., Marekani. Mikutano hiyo, iliyobeba kaulimbiu “Ajira: Njia ya Mafanikio”, ilikusanya viongozi waandamizi wa fedha kutoka nchi wanachama kujadili maendeleo ya kiuchumi duniani, changamoto zinazoikabili jamii ya kimataifa, na fursa za ushirikiano wa kifedha.
Gavana Tutuba alishiriki mikutano hiyo pamoja na Naibu Gavana wa BoT, Dkt. Yamungu Kayandabila, wakiwa sehemu ya ujumbe rasmi wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), ambaye pia ni Gavana wa Benki ya Dunia kwa upande wa Tanzania.
Katika mkutano huo, Gavana Tutuba alihudhuria vikao muhimu vikiwemo vya viongozi wa taasisi za fedha na sekta binafsi, ambapo alielezea mafanikio ya Tanzania katika kuimarisha mfumo wa fedha na hatua za serikali katika kukuza uchumi jumuishi unaojikita katika matumizi ya teknolojia ya kifedha (fintech). Pia alihimiza mashirikiano ya kimataifa katika kupunguza gharama za miamala ya kifedha na kuongeza upatikanaji wa huduma rasmi kwa wananchi.
Sambamba na mikutano hiyo, Gavana Tutuba alikutana na Rais wa Kampuni ya VISA anayesimamia Ukanda wa Ulaya ya Kati, Mashariki ya Kati na Afrika, Bw. Andrew Torre, ambapo walijadili mikakati ya kupunguza matumizi ya fedha taslimu nchini kwa kukuza huduma za malipo ya kidigitali. VISA ilieleza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na BoT katika kutoa mafunzo na kuimarisha mifumo salama ya malipo.
Aidha, Gavana Tutuba alishiriki katika Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu za Afrika uliofanyika katika Ofisi za Kamisheni ya Umoja wa Afrika, kwa lengo la kujadili ajenda za pamoja ambazo Afrika inaweza kuwasilisha kwa umoja katika mikutano ya Kundi la Nchi 20 Tajiri Duniani (G20) mwaka 2025, ambapo Afrika Kusini ni Mwenyekiti. Mkutano huo uliangazia umuhimu wa Afrika kuwa na sauti ya pamoja katika kushawishi mabadiliko ya sera za kimataifa ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo nafuu na kupunguza mzigo wa madeni kwa mataifa yanayoendelea.
Katika kikao kingine muhimu, Gavana Tutuba alishiriki mazungumzo kati ya ujumbe wa Tanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Adran Ubisse. Mazungumzo hayo yalilenga kujadili athari za mabadiliko ya sera za Marekani dhidi ya nchi za Afrika, ambapo Tanzania ilisisitiza nia ya kujitegemea kwa kutumia rasilimali za ndani kupitia Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Ushiriki wa Gavana Tutuba katika mikutano hii umeonesha dhamira ya Benki Kuu ya Tanzania kuimarisha nafasi yake katika majukwaa ya kimataifa na kuchangia katika mijadala ya sera za kifedha zenye lengo la kukuza uchumi shirikishi, unaojibu changamoto za sasa na kuandaa msingi wa maendeleo endelevu kwa wananchi wote.