Skip to content
BoT yaiwakilisha NGFS katika mjadala wa kimataifa kuhusu Misitu na Uthabiti wa Kiuchumi

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikiwa ni mwanachama hai wa Mtandao wa Benki Kuu na Mamlaka za Usimamizi wa Sekta ya Fedha kwa ajili ya Kuhamasisha Mfumo wa Fedha Rafiki kwa Mazingira (NGFS), imeiwakilisha taasisi hiyo katika mjadala wa ngazi ya juu uliopewa jina la “Too Big to Fail: Forests as Macro-Critical Assets”.

Mjadala huo ulifanyika tarehe 17 Novemba 2026 jijini Antalya, Uturuki, pembezoni mwa Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31).

Akiwakilisha BoT na NGFS, Mchambuzi wa Masuala ya Fedha, Mabadiliko ya Tabianchi na Uendelevu kutoka BoT, Bw. Joseph Paul Kenene, alibainisha nafasi ya benki kuu duniani katika kutambua na kudhibiti vihatarishi vya kiuchumi na kifedha vinavyotokana na ukataji miti, uharibifu wa misitu na kupungua kwa bioanuai.

Alieleza kuwa misitu si rasilimali ya kimazingira pekee, bali ni nguzo muhimu ya uthabiti wa uchumi mpana na sekta ya fedha. Misitu hutoa huduma za kiikolojia kama udhibiti wa tabianchi, uhifadhi wa vyanzo vya maji na udongo ambazo ni tegemeo kuu kwa sekta za kilimo, nishati na utalii; hivyo uharibifu wake huleta madhara ya moja kwa moja kwa biashara na benki.

Aidha, Bw. Kenene alisisitiza kuwa taasisi za fedha zinapaswa kutambua namna shughuli zao zinavyotegemea na kuathiri mazingira asilia, na kutathmini jinsi uharibifu wa ikolojia unavyoweza kuibua vihatarishi vya mikopo, masoko na uendeshaji.

Alitaja hatua za kimkakati ambazo benki kuu zinaweza kuchukua ndani ya mamlaka yao ya kisheria, zikiwemo kuimarisha tathmini ya vihatarishi vya kimazingira, kuboresha upatikanaji wa takwimu, kujenga uwezo wa kitaasisi, na kuchochea ufadhili endelevu katika uhifadhi wa misitu na matumizi bora ya ardhi.

Mjadala huo uliandaliwa na taasisi ya Global Optimism kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Ushirikiano wa Viongozi kuhusu Misitu na Tabianchi (Forest and Climate Leaders’ Partnership – FCLP). Uliwakutanisha viongozi wa serikali, Benki ya Dunia, benki kuu mbalimbali na wawekezaji ili kuongeza kasi ya kufanikisha lengo la kimataifa la kusitisha uharibifu wa misitu ifikapo mwaka 2030.