Mifuko ya udhamini wa mikopo
Muhtasari

Mageuzi katika sekta ya fedha ya mwaka 1991 yalisaidia kujenga mazingira bora ya soko huria na kuboresha huduma za kifedha nchini. Hata hivyo, upatikanaji wa mikopo, hasa kwenye sekta ya kilimo na kwa wajasiriamali wadogo na wa kati ilibaki kuwa changamoto.

Katika jitihada za kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania ilianzisha Mfuko wa Udhamini wa Mikopo unaolenga kukuza na kusaidia sekta binafsi kwa kuweka mazingira wezeshi ya kupanua na kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha na mitaji, ili kuchochea ajira na mauzo nje ya Nchi; hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi.

Benki Kuu kwa niaba ya Serikali inasimamia Mifuko miwili ya Udhamini wa Mikopo ambayo ni:

  1. Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa ajili ya Mauzo Nje ya Nchi (ECGS):

    Mfuko huu ulianzishwa Julai 2002 kwa lengo la kuwezesha wakopaji wenye miradi mizuri kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa na mauzo nje ya nchi, kuweza kupata mitaji kutoka kwenye mabenki na taasisi za fedha, pale wanapokuwa na upungufu wa dhamana.

    Udhamini wa mikopo katika Mfuko huu hauzidi asilimia 75 kwa mkopo unaolipika ndani ya mwaka mmoja; na asimilia 50 ya mkopo kwa mkopo unaolipika zaidi ya mwaka mmoja. Vilevile, kwa mkopo wa mazao ambayo mzunguko wa uzalishaji na uuzaji wake unazidi miezi kumi na mbili (12) lakini si zaidi ya miezi kumi na tano (15), udhamini wa mkopo hautazidi asilimia 75.

  2. Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SME-CGS):

    Mfuko huu ulianzishwa Septemba 2005 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati wenye miradi mizuri lakini wana upungufu wa dhamana, kuweza kupata mitaji kutoka kwenye mabenki na taasisi za fedha.

    Mfuko huu unatoa udhamini usiozidi asilimia 50 kwa mikopo kati ya shilingi milioni 50 hadi shilingi bilioni 1.0 itakayotolewa kwa kipindi kati ya mwaka 1 hadi 5. Aidha udhamini wa mkopo utakaotolewa kwenye mifuko hii utakuwa kwenye deni kuu tu hivyo hautahusisha riba katika kipindi chote cha mkopo.


Vigezo Vya Kupata Udhamini
  1. Mkopaji
    • biashara iliyosajiliwa na inayofanya kazi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumilikiwa na raia wengi wa Tanzania;
    • biashara inayoshughulika na uzalishaji na/au uongezaji wa thamani kwa mauzo ya nje, vilevile mradi huu uwe umepitia tathmini ya kina ya mikopo ya taasisi ya fedha na kukidhi sifa;
    • biashara inayoweza kutengeneza ajira, kuzalisha mapato ya kodi hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
    • usimamizi na utaalamu wa kuaminika katika aina ya biashara ambayo dhamana inaombwa;
    • mchango wa mtaji katika mradi au biashara husika, unaokidhi matakwa ya taasisi ya fedha; na
    • uwezo kutoa dhamana yoyote inayoweza kutekelezeka ikijumuisha dhamana ya kibinafsi na dhamana ya watu wengine. Kiwango na aina ya dhamana itakayotolewa itaamuliwa na taasisi ya fedha.
  2. Mradi
    • Biashara inayoshughulika na uzalishaji na/au uongezaji wa thamani kwa mauzo ya nje, vilevile mradi huu uwe umepitia tathmini ya kina ya mikopo ya taasisi ya fedha na kukidhi vigezo sifa; na
    • Mradi unaoanza au unaoendelea.
  3. Benki na taasisi za fedha shiriki
    Mabenki na taasisi za fedha zote zilizosajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania zinaweza kushiriki katika mifuko hii ya udhamini wa mikopo.
Taratibu za Uombaji

Waombaji wanapaswa kupeleka maombi ya mikopo moja kwa moja katika benki au taasisi ya fedha zilizosajiliwa chini ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya Mwaka 2006. Baada ya kuchagua benki au taasisi ya fedha, muombaji atapeleka upembuzi yakinifu wa mradi wake na mahitaji mengine kulingana na benki au taasisi ya fedha itakavyoelekeza.

Benki au taasisi ya fedha itafuata taratibu zote za kibenki kabla ya kupitisha mkopo, ikiwa ni pamoja na upembuzi yakinifu wa mradi husika, kuangalia taarifa za muombaji kuhusu taarifa ya mikopo mingine, aliyowahi kupata na kusajiliwa (Credit Reference Bureau).

Baada ya benki au taasisi ya fedha husika kuridhika na mradi wa muombaji, maombi yatawasilishwa Benki Kuu ya Tanzania kwa udhamini kupitia fomu maalum ilianishwa kwa mfuko husika. fomu ya maombi ya udhamini wa mkopo – SME-CGS/ECGS)

Benki Kuu itashughulikia maombi ya udhamini kulingana na taratibu na miongozo ya usimamizi wa mifuko ya udhamini wa mikopo na kuzingatia kama maombi yamekisdhi vigezo vilivyoainishwa katika miongozo yote. Endapo masharti na vigezo vikitimizwa Benki Kuu kwa niaba ya Serikali itatoa udhamini kwa benki au taasisi husika ya fedha ili iweze kutoa mkopo kwa mwombaji.

Baada ya udhamini kutolewa, benki au taasisi ya fedha husika inawajibika kufuatilia maendeleo ya mradi na marejesho na kuwasilisha taarifa Benki Kuu.