Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amekutana na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Mhe. Christine Grau, katika Ofisi za Benki Kuu jijini Dar es Salaam na kujadiliana masuala mbalimbali kuhusu uchumi wa nchi yetu.
Katika kikao hicho, Gavana Tutuba ameelezea hatua zilizochukuliwa na BoT katika kuanza kwa mfumo wa utekelezaji wa sera ya fedha unaotumia riba ambapo Kamati ya Sera ya Fedha imetangaza Riba ya Benki Kuu kuwa asilimia 5.5 kwa robo ya kwanza ya mwaka huu. Amesema mfumo huo unalenga kuongeza ufanisi wa sera ya fedha ili kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Gavana pia amezungumzia kuhusu jitihada zinazofanywa na serikali katika kukuza huduma jumuishi za fedha nchini ambapo hivi karibuni akiwa kama Mwenyekiti wa Baraza la Huduma Jumuishi za Fedha amezindua Mtaala wa Wakufunzi wa Elimu ya Fedha unaolenga kutatua changamoto zitokanazo na upungufu wa ujuzi wa usimamizi binafsi wa masuala ya fedha.
Aidha, Gavana ameuomba Umoja wa Ulaya kuwajengea uwezo zaidi wafanyakazi wa BoT na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya fedha na uchumi ili waweze kutimiza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Gavana amesema kuwa BoT inathamini ushirikiano na Umoja wa Ulaya katika kusaidia maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi nchini na kuongeza kuwa BoT itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Umoja huo katika masuala ya pamoja.
Kwa upande wake, Balozi Grau amempongeza Gavana kwa juhudi zake za kusimamia na kuboresha sekta ya fedha na uchumi nchini na kusema kuwa Umoja wa Ulaya uko tayari kushirikiana na BoT katika kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa BoT.
Balozi pia amesema kuwa Umoja wa Ulaya unaunga mkono jitihada za BoT katika kutekeleza mfumo wa utekelezaji wa sera ya fedha unaotumia riba, kuendeleza huduma jumuishi za fedha na kuboresha mifumo ya malipo.
Balozi amesema kuwa Umoja wa Ulaya unatambua umuhimu wa sekta ya fedha na uchumi katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu na kutoa fursa kwa wananchi.