Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel M. Tutuba, ameungana na magavana wengine wa benki kuu na mawaziri wa fedha kutoka nchi takribani 190, wabunge, wakuu wa sekta binafsi, wawakilishi kutoka mashirika ya kiraia, na wanazuoni katika mkutano wa kila mwaka wa Benki ya Dunia/ Shirika la Fedha la Kimataifa (WB/IMF) - 2023 unaofanyika huko Marrakech, Morocco, kuanzia tarehe 9 hadi 15 Oktoba 2023. Katika Mkutano huo masuala mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo matarajio ya uchumi wa dunia, utokomezaji wa umaskini, maendeleo ya uchumi, na ufanisi wa misaada itolewayo na mashirika haya.
Kabla ya mkutano huo wa WB/IMF wa mwaka 2023, Gavana Tutuba alihudhuria mkutano wa pamoja wa wajumbe wa Taasisi ya Usimamizi wa Uchumi Mpana na Sekta ya Fedha Mashariki na Kusini mwa Afrika (MEFMI) uliofanyika tarehe 8 Oktoba 2023 huko Marrakech, Morocco. Mkutano huo hufanyika kila mwaka kabla ya mikutano ya mwisho wa mwaka ya WB/IMF na hujumuisha mawaziri na makatibu wakuu wa wizara za fedha na mipango pamoja na magavana wa benki kuu za nchi wanachama 14 za MEFMI. Mada iliyojadiliwa mwaka huu ni “Mabadiliko ya Tabia nchi na Benki Kuu."
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya MEFMI, Dk. Louis Kasekende, a
kiwakaribisha wajumbe katika mkutano huo alisema “Mabadiliko ya tabia nchi ni janga kubwa hususan katika maendeleo ya uchumi. Katika siku za hivi karibuni, tumeshuhudia majanga makubwa yaliyosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi yaliyosababisha upotevu wa maisha, uharibifu wa mali na miundo mbinu na hivyo kuathiri uchumi wa dunia ikiwemo nchi wanachama wa MEFMI.”
Kwa niaba ya Bodi ya Magavana, uongozi na wafanyakazi wote wa MEFMI, Dk. Kasekende ametoa pole kwa Falme ya Morocco kufuatia athari za tetemeko la ardhi lililotokea hivi karibuni. “Tunaomba Mwenyezi Mungu awajalie majeruhi wa tetemeko hili uponywaji wa haraka na pia kuiwezesha nchi iweze kurudia hali yake ya uchumi kama ilivyokua awali.”
Akizungumza katika Mkutano wa pamoja wa MEFMI wa Mwaka 2023, Mshauri Mkuu wa Kundi la Benki ya Biashara na Maendeleo (TDB Group), Reginald Max, aliwataka washiriki kutumia fursa hiyo kufafanua upya jukumu la benki kuu na wizara za fedha kama wasimamizi wa mustakabali wetu wa kiuchumi na mazingira.
"Kama mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu, tunabeba jukumu kubwa la kulinda na kukuza ustawi wa kiuchumi wa nchi zetu. Walakini, mbele ya mabadiliko ya hali ya hewa, majukumu yetu ya kawaida lazima yabadilike," alisema.
Aliongeza kuwa Afrika daima imekuwa ikijulikana kwa ustahimilivu wake, na pamoja, tunaweza kushinda changamoto zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.