Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, ametembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwenye sherehe za ufungaji wa Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita na kupokelewa na Naibu Gavana wa BoT, Dkt. Yamungu Kayandabila.
Dkt. Kayandabila alifafanua juu ya juhudi za BoT katika kuendeleza uchumi wa nchi kupitia sekta ya madini. Alisema kuwa BoT imeanzisha Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Ajili ya Mauzo ya Bidhaa za Nje ya Nchi, maarufu kama Export Credit Guarantee Scheme. Mfuko huu unalenga kutoa udhamini wa mikopo kwa wachimbaji wadogo na wakati, lengo likiwa ni kuwawezesha kuongeza uzalishaji wa dhahabu.
“Mfuko huu ni sehemu ya jitihada za serikali na BoT katika kukuza sekta ya madini utakaoiwezesha BoT kupata dhahabu ya kutosha itakayohifadhiwa kama akiba ya nchi ya fedha za kigeni na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania,” alisema Dkt. Kayandabila
Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini, ambayo yamefanyika kuanzia tarehe 20 hadi 30 Septemba, 2023, katika viwanja vya Bomba mbili mkoani Geita, yamekuwa jukwaa la kipekee kwa wadau wa sekta ya madini kutoka ndani na nje ya nchi kubadilishana mawazo, teknolojia, na uzoefu wa kisasa katika uchimbaji wa madini.