GAVANA BOT AWASIHI WADAU KUUNGANA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA UCHUMI DUNIANI

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amewasihi wadau katika sekta ya uchumi na fedha kuungana ili kukabiliana na changamoto za kiuchumi duniani. Gavana Tutuba, alisema hivyo katika mkutano na Jumuiya ya Biashara ya Uswisi na Tanzania (Switzerland Tanzania Chamber of Commerce) ambapo masuala kadhaa yalijadiliwa, ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa biashara, kuongeza fursa za uwekezaji nchini, njia za ushirikiano wa kifedha, na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kushughulikia baadhi ya changamoto zinazokabili uchumi wa dunia ikiwa ni pamoja na Tanzania.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Biashara ya Uswisi na Tanzania, Bi. Amne Suedi, aliipongeza jitihada za BoT  katika kuimarisha sekta ya uchumi na fedha  inayovutia uwekezaji nchini.

Licha ya changamoto zinazokabili uchumi wa dunia, Gavana amesisitiza kuwa Tanzania ni eneo bora kwa ajili ya uwekezaji. Aidha, Gavana Tutuba, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Uswisi uliyodumu kwa muda mrefu.