Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, anashiriki Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Jukwaa la Wakuu wa Taasisi za Umma.
Kikao hicho ambacho kilifunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kinafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha kuanzia tarehe 19 - 21 Agosti, 2023.
Ajenda mbalimbali, zikiwemo mada tano muhimu za kuboresha zaidi utendaji wa taasisi za umma, zinajadiliwa. Vile vile, Kikao kazi hicho kinapitia na kujadili Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, maboresho ya usimamizi wa taasisi na kutoa vigezo vya utendaji kazi ambapo taasisi hizo zitapatiwa vigezo vipya vya kufanyia kazi kulingana na sekta husika.
Pia, kitajadili changamoto mbalimbali za taasisi, zikiwemo za viongozi hao na kupatiwa mafunzo ya uongozi ili kuboresha utendaji wa taasisi.