Gavana Tutuba aangazia nguvu ya teknolojia ya fedha kukuza uchumi

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, amesema kuwa teknolojia ya fedha inamchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, akieleza kuwa inaongeza kasi ya miamala, inapunguza gharama za huduma na kuwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa watu wengi zaidi, wakiwemo walioko maeneo ya mbali. 

Gavana Tutuba ameyasema hayo alipokuwa akichangia katika mjadala wa mawaziri wakati wa Kikao cha 58 cha Tume ya Uchumi ya Afrika (ECA), kinachofanyika jijini Tangier, Morocco, kuanzia tarehe 28 Machi hadi 3 Aprili 2026. Kikao hicho kimewakutanisha Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi pamoja na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi mbalimbali za Afrika, kujadili mwelekeo wa uchumi wa bara hilo.

Katika mchango wake, Gavana Tutuba amebainisha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika ujumuishaji wa kifedha kupitia huduma za fedha kwa njia ya simu na mifumo ya malipo yakidigitali yenye ufanisi. Amesema mafanikio hayo yamechangia kupunguza gharama za miamala, kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya serikali na kuongeza uwazi katika matumizi ya fedha.

Aidha, ameeleza kuwa Tanzania ni sehemu ya mifumo ya malipo ya kikanda ikiwemo Mfumo wa Malipo wa Afrika Mashariki (EAPS) na Mfumo wa Malipo wa Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC RTGS). Vilevile, amebainisha kuwa benki za biashara nchini zinaendelea kujiunga na Mfumo wa Malipo wa Afrika (PAPSS), unaowezesha miamala ya kifedha kati ya nchi za Afrika kwa haraka na ufanisi, hatua itakayochochea biashara na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika.

Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2050, Gavana Tutuba amesisitiza kuwa teknolojia ya fedha pamoja na teknolojia nyingine za kidijitali zitaendelea kuwa nguzo muhimu katika kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani.

Katika kukuza ubunifu, Gavana ameeleza kuwa Benki Kuu ya Tanzania inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana wabunifu kupitia majukwaa mbalimbali ya ubunifu ili kuibua suluhisho za kidijitali zitakazoboresha huduma za kifedha.

Vilevile, amesema Benki Kuu inaendelea kutumia akili unde (AI) na imesaini makubaliano na vyuo vikuu mbalimbali nchini kwa lengo la kuendeleza tafiti zitakazosaidia matumizi mapana ya teknolojia hiyo katika sekta ya fedha.