Masoko ya Fedha
Benki Kuu ya Tanzania ina mchango mkubwa katika maendeleo ya masoko ya fedha nchini kwa kujenga mazingira wezeshi. Mchango wa Benki Kuu imejikita hasa katika kutoa miundombinu ya masoko ya fedha, kuhakikisha kuna sheria zinazotakiwa, kusimamia na kujenga nyenzo za masoko. Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, 1995 ilitoa mwanya wa kuanzisha masoko ya fedha nchini. Masoko ya fedha nchini yanahusisha fedha na zana masoko ya mitaji yanafanyika katika minada ya awali na ya upili. Kurugenzi ya Masoko ya Fedha ina jukumu la kutekeleza sera ya fedha ya Benki Kuu na kusimamia akiba ya taifa ya fedha za kigeni. Pia, inasimamia minada ya dhamana za serikali.

Matukio makubwa katika Masoko ya Fedha Tanzania

 • Novemba 2018:Kuanzishwa kwa Mfumo wa Soko la Fedha la Mabenki -IBCM
 • Septemba 2018:Kuanzishwa kwa Dhamana ya Serikali ya miaka 20 yenye lengo la kurefusha muda wa kuiva kwa dhamana za serikali.
 • Julai 2017:Kuunganishwa kwa Mfumo Mkuu wa BoT (BOT Central Depository System) na Mfumo Mkuu wa Dhamana wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE Central Securities System).
 • Novemba 2013: Kuanzishwa kwa Dhamana ya Serikali ya miaka 15- yenye lengo la kurefusha muda wa kuiva kwa dhamana za serikali.
 • Augusti 2012:Kuanzishwa kwa Washiriki Wakuu katika Minada ya Dhamana za Serikali (Central Depository Participants (CDPs)) na ushiriki katika minada ya dhamana za serikali kwa njia ya mtandao.
 • Januari 2008: Uoanishi wa malipo ya Dhamana za Serikali kwa muda wa siku moja (Harmonization of redemption and settlement of Government securities to T+1).
 • Januari 2008: Utaratibu wa kuendesha minada ya hati fungani za muda mfupi kila wiki ulibadilishwa na kuanza kufanya minada hiyo kila baada ya wiki mbili na ile minada ya Hati Fungani za muda mrefu ilibadilishwa na kuwa inafanyika mara moja kwa mwezi.
 • Machi 2004: Jukwaa la Viongozi wa Masoko ya Fedha lilianzishwa in kukuza mijadala na mtandao miongoni mwa wadau katika masoko ya fedha. Kupitia Jukwaa hilo, wadau wamekuwa wakibadilishana ujuzi kaika vikao rasmi na visivyo rasmi na kusaidia kuongeza uelewa jinsi masoko yanavyoendeshwa miongoni mwa washiriki.
 • Desemba 2003: Benki Kuu ilianzisha mikopo siku moja na kati ya siku 7 na 14 (Intraday and Lombard standby credit facilities) ili kuzipatia benki mikopo kwa ajili kutatua mahitaji ya muda mfupi ya fedha.
 • Mei 2003: Serikali iliruhusu wawekezaji wa kigeni katika Soko la Hisa la Dar es Salaam. Kanuni mbalimbali zilitungwa mwaka 2003 kama mwongozo kwa wawekezaji wanje katika Soko la Hisa pamoja na kuweka udhibiti ili soko liendeshwe kwa utaratibu mzuri.
 • Oktoba 2002: Wizara ya Fedha ilitoa kiasi cha ziada cha dhamana cha shilingi bilioni 80.0 kwenye soko la dhamana za serikali (additional non-marketable stocks).
 • Agosti 2002: Kwa niaba ya serikali, Benki Kuu ilizindua Hati Fungani ya miaka 10.
 • Julai 2002: Benki Kuu ilianzisha Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa ajili ya Kuuza nje ili kuharakisha upatikanaji wa mikopo kwa sekta ya wawekezaji kwa ajili ya kuuza nje, hasa bidhaa zisizo za asili ili kuongeza wigo wa mapato ya fedha za kigeni.
 • Julai 2002: Wizara ya Fedha ilitoa nyongeza ya shilingi bilioni 20.0 ya madeni ya ndani kisicho na dhamana ili kunadiwa katika soko la dhamana za serikali (additional unsecuritized domestic debts).
 • Julai 2002: Benki Kuu ya Tanzania, kwa niaba ya serikali, ilianza kuuza Hati fungani ya miaka 7.
 • Mei 2002: Benki Kuu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, ilibadilisha madeni ya ndani yasiyo na dhamana ya shilingi bilioni 20.0 kuwa dhamana zinazoweza kuuzwa.
 • Mei 2002: Benki Kuu ilianzisha tena kunadi hati fungani ya siku 35 kama nyenzo ya sera ya fedha.
 • Aprili 2002: Benki Kuu ya Tanzania ilibadilisha utaratibu wa kuwa na bei moja (unifom prices) kwa hati fungani ya miaka miwili na kuruhusu bei tofauti (multiple prices).
 • Februari 2002: Benki Kuu ya Tanzania kwa niaba ya serikali Ilianza kuuza Hati Fungani ya miaka 5. Hati fungani hii imesajiliwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam. Lengo la dhamana ya miaka 5 ni kupanga vizuri namna madeni ya serikali yanavyoiva, kuongeza muda wa kuiva kwa dhamana hiyo na kuongeza idadi ya nyenzo katika soko.
 • Julai 1999: Benki Kuu ya Tanzania ilianzishwa mfumo wa kuweka kumbukumbu za wawekezaji kwenye dhamana za serikali za muda mfupi kwa njia ya kompyuta (Central Depository System for Treasury bills). Mfumo huu unahusu kuweka kumbukumbu, kuhamisha na kuboresha umiliki wa hati fungani za muda mfupi bila kulazimika kutoa hati za karatasi za umiliki na hivyo kuongeza ufanisi. Mfumo huu unawezesha kugawa dhamana zilizowekezwa katika vipande vidogo vidogo na kukuza biashara katika soko la upili.
 • Aprili 1998: Biashara ya hisa ilianza katika Soko la Hisa la Dar es Salaam baada ya kukamilika maandalizi ya miaka miwili chini ya usimamizi wa serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana. Kuanza kwa uuzaji wa hisa ulienda sambamba na kuandikishwa kwa TOL Limited (zamani ikiitwa Tanzania Oxygen Limited), kama kampuni a kwanza katika soko hilo.
 • Septemba 1996: Soko la Hisa la Dar es Salaam lilianzishwa kama kampuni binafsi (private company limited by guarantee and not having a share capital) kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni.
 • Julai 1997: Utaratibu wa mikataba ya kukopeshana baina ya mabenki (Repurchase agreements) ilianzishwa kama zana ya ziada pamoja na hati fungani za muda mfupi na muda mrefu katika uendeshaji wa soko huru.
 • 1996: Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ilianzishwa ili kuwezesha uanzishwaji wa soko la hisa kwa ajili ya kukusanya fedha kwa ajili ya uwekezaji wa muda wa kati na muda mrefu.
 • Desemba 1994: Mnada wa Hati Fungani za muda mfupi wa siku 364 ulianzishwa rasmi tarehe 7 Desemba 1994.
 • Desemba 1994: Mnada wa hati fungani ya siku 35 ulisitishwa.
 • 1994 Kurugenzi ya Masoko ya Fedha ilianzishwa ili kuendeleza na kusimamia masoko ya fedha.
 • Juni, 1994: soko la fedha za kigeni kati ya mabenki (IFEM) lilianzishwa badala ya mfumo wa mnada wa fedha za kigeni uliokuwa unafanyika mara moja kwa wiki. IFEM ni soko la jumla ambalo liliwezesha kuamua kiwango cha kubadilisha fedha za kigeni.
 • Februari 1994: Mnada wa Hati Fungani ya siku 182 ulianza.
 • Januari 1994: Sheria ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana yam waka 1994 ilitungwa.
 • Septemba 1993: Minada wa Hati Fungani ya siku 35.
 • Agosti 1993: Benki Kuu ilianza kutumia hati fungani za muda mfupi kama njia ya kugharamia shughuli za serikali kwa muda mfupi na kudhibiti fedha katika mzunguko; pia zilitumika kama kigezo cha kuweka kiwango cha riba ya kukopeshana. Benki Kuu ilianza kuwa kuuza hati fungani za siku 91.
 • Julai 1993: Benki Kuu ilianza kuuza fedha za kigeni kwa njia ya mnada kama njia ya kudhibiti fedha katika mzunguko na kama kiashiria cha kuamua kiwango cha kubadiisha fedha
 • Juni 1993: Benki Kuu ya Tanzania ilitoa hati ya amana (Certificate of Deposit) kama zana ya sera ya fedha.
 • Aprili 1993: Kuruhusiwa kwa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni katika jitihada za kufunguza milango ya kubadilisha fedha za kigeni.
 • Machi 1992: Sheria ya Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 ilitungwa. Sheria hii iliruhusu biashara ya fedha za kigeni na kuweka mazingira ya kutumia kupata kiwango cha kubadilisha fedha za kigeni kwa nguvu ya soko.