Akiba ya Fedha za Kigeni

Akiba ya fedha za kigeni inasimamiwa kwa mujibu wa sera za uwekezaji zilizopitishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu ya Tanzania. Benki Kuu huhifadhi akiba ya taifa ya fedha za kigeni kwa mujibu wa vifungu vya 51 na 52 vya Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, 2006.

Masoko ya fedha yanalenga kuhakikisha kwamba Benki Kuu inalinda mtaji wake, kutosheleza mahitaji ya ukwasi na kuongeza mapato kulingana na uwezo wa mazingira ya soko.. Mchanganyiko wa akiba ya fedha za kigeni hupangwa kuendana na uwiano wa mahitaji ya fedha za kigeni kwa ajili ya kulipia madeni ya nje, mahitaji ya bidhaa na huduma kutoka nje pamoja na mahitaji mengine ya fedha za kigeni yasiyohusiana na uagizaji wa bidhaa na huduma.

Sababu za kuwa na akiba ya fedha za kigeni ni:

  • Kuiwezesha serikali kutimiza mahitaji yake ya fedha za kigeni na mahitaji ya kuagiza bidhaa kutoka nje,
  • Kutoa imani kwamba serikali inaweza ikatimiza majukumu yake ya muda mfupi kulipa madeni ya nje,
  • Kusaidia utekelezaji wa sera za fedha na kubadilisha fedha za kigeni, pamoja na uwezo wa kuingilia kuhakikisha fedha ya taifa ni imara,
  • Kuchangia katika mapato ya Benki Kuu kwa kuhakikisha kuna kiwango cha kutosha cha mapato kulingana na jinsi Benki inavyoweza kuhimili majanga/vihatarishi.

Usimamizi wa Akiba ya Fedha za Kigeni

Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, 2006 inaitaka Benki Kuu kutunza akiba ya fedha za kigeni ambayo inaweza kukidhi mahitaji ya huduma na bidhaa kutoka nje kwa angalau kipindi cha miezi minne pamoja na mahitaji mengine ya miamala ya kimataifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi hicho hicho.. Akiba ya fedha za kigeni hutumika:

  • Kulipia madeni ya nje ya serikali na sekta binafsi.
  • Kuingilia katika soko la ndani la fedha za kigeni ili kuleta utulivu pale ambapo haupo pamoja an kufanya malipo fedha za kigeni ya Benki Kuu ya Tanzania.
  • Kama kinga dhidi ya majanga yanayoweza kutokea huko nje na mambo mengine.

Kiwango cha akiba rasmi ya fedha za kigeni kinachenga imani kwa wawekezaji watarajiwa, taasisi za kupima viwango (rating agencies) na watu wanaofikiria kutoa fedha zao za kigeni kutoka hapa nchini.. Ili kuhakikisha usimamizi mzuri wa akiba ya fedha za kigeni, malengo ya sera ya fedha za kigeni ya Benki Kuu ni: Kutunza mtaji, Ukwasi na Kupata kipato.