Deni la Ndani la Serikali

Soko la Dhamana za Serikali za Muda Mfupi

Hatifungani za muda mfupi ni dhamana za serikali za muda mfupi ambazo hutolewa na kuiva chini ya mwaka mmoja. Hatifungani za muda mfupi zinatumika kama zana za muda mfupi kupata fedha kwa ajili ya kuziba mapungufu katika bajeti na kusawazisha ujazi wa fedha katika soko. Kwa sasa, Benki Kuu hunadi hatifungani za muda mfupi kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, hatifungani za muda mfupi ziko za aina nne – zinazoiva katika kipindi cha siku 35, siku 91, siku 182 na siku 364. Kiwango cha chini cha uwekezaji katika dhamana za muda mfupi ni shilingi 500,000 (Shilingi Laki Tano katika mafungu ya shilingi 10,000).

Soko la Dhamana za Serikali za Muda Mrefu

Hatifungani za muda mrefu ni zile ambazo zinaiva katika kipindi zaidi ya mwaka mmoja na kulipa riba kila nusu mwaka. Hatifungani za muda mrefu zinazotolewa na Benki Kuu ya Tanzania huiva katika kipindi cha miaka 2, miaka 5, 7, 10, 15 na miaka 20. Zinatolewa kwa riba iliyopangwa (kuponi). Kiwango cha chini cha uwekezaji katika hatifungani za muda mrefu ni shilingi 1,000,000 (Shilingi milioni moja) katika mafungu ya shilingi 100,000. Wawekezaji hutaja bei ya juu, inayofanana na kiwango kinachotolewa au ya chini (quoted at either Premium, Par or Discount). Kama fursa za uwekezaji, Hatifungani za Muda Mrefu na za Muda Mfupi zina faida zifuatazo:
    • Ni njia salama na rahisi ya umilikaji wa dhamana hizi ukilinganisha na mfumo wa umiliki kwa kutumia hati.
    • Zinaweza kubadilishwa umiliki.
    • Zinaweza kutumika kama dhamana.
    • Kipato chake ni kizuri.