Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Sera za Uchumi na Fedha), Dkt. Yamungu Kayandabila, amefungua semina ya waandishi wa habari kwa kuvishukuru vyombo vya habari kwa ushirikiano wao katika kuuhabarisha umma.
Amewaambia washiriki 34 wa semina hiyo inayofanyika katika ofisi Ndogo za Makao Makuu ya BoT Zanzibar kwamba Benki Kuu ya Tanzania inaridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na vyombo vya habari hapa nchini katika kutoa taarifa kwa umma.
Amesema Benki Kuu inafikiria njia sahihi za kujengeana uwezo, lakini pia kupata mrejesho kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu utendaji kazi wake.
Katika semina ya mwaka huu inayofanyika kuanzia tarehe 14 – 16 Februari 2024, washiriki watajifunza kuhusu mfumo mpya wa Sera ya Fedha unaotumia Riba ya Benki Kuu ambao umeanza kutumika kuanzia Januari mwaka huu; utekelezaji wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, ikiwemo masuala ya mikopo; namna Benki Kuu inavyomlinda mtumiaji wa huduma za fedha; na faida za kutumia mifumo mbadala ya malipo badala ya pesa taslimu.
“Tunaamini kupitia mada hizo tutaweza kuchangia kuongeza uelewa wenu kuhusu kazi za Benki Kuu kama nyenzo yenu ya kazi ili muweze kuwa na uwanja mpana wa kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala hayo kupitia vyombo vyenu vya habari,” amesema Dkt. Kayandabila
Amevishukuru vyombo vya habari nchini kwa kuendelea kutoa uzito kwa masuala ya fedha, biashara na uchumi kwa kuwa na habari, makala, vipindi maalum na mahojiano. Kwa kufanya hivyo, Naibu Gavana amesema, vyombo vya habari ni daraja muhimu kati ya wananchi na taasisi za fedha, ikiwemo Benki Kuu.
Akizungumzia mfumo mpya wa kuandaa na kutekeleza sera ya fedha, amesema, mfumo huo unatarajia kuongeza ufanisi wa sera ya fedha katika kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha shughuli za kiuchumi.
“Mfumo huu utawezesha Benki Kuu ya Tanzania kurekebisha riba kulingana na hali ya uchumi na kuhakikisha kwamba kuna usawa kati ya mahitaji na usambazaji wa fedha,” amesema.
Pia mfumo huo utasaidia kuzuia kupanda kwa bei za bidhaa na huduma, ambazo zinaweza kupunguza nguvu ya ununuzi wa wananchi na kudhoofisha ukuaji wa Uchumi, amesema Dkt. Kayandabila.
Katika ufunguzi huo, walikuwepo pia Kaimu Mkurugenzi wa BoT Zanzibar, Bw. Masoud Suleiman na Meneja wa BoT Idara ya Mawasiliano, Bi. Victoria Msina.