Benki Kuu za EAC zaungana kukabili Mabadiliko ya Tabianchi na Kidijitali

Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania kimeandaa kozi ya kikanda ya siku tano kuanzia Februari 5 hadi 9, 2024 jijini Arusha katika jitihada za kukabiliana na changamoto zinazosababishwana mabadiliko ya tabianchi na kidijitali katika sekta ya kifedha.

Washiriki wa kozi hiyo wanatoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), benki kuu katika kanda hii,  na mashirika ya kimataifa.

Kozi hiyo imefanikishwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Dunia, Taasisi ya kuangalia masuala ya tabianchi katika mfumo wa Fedha (NGFS), Kituo cha Rasilimali cha Usalama wa Mtandao wa Afrika (ACRC), Umoja wa Fedha wa Afrika Magharibi (WAMU), na Taasisi ya Kimataifa ya Sera za Ustahimilivu wa Uchumi (GIMM). Inalenga kuhamasisha kubadilishana maarifa na kushirikiana katika kukabiliana na changamoto za pamoja.

Akifungua mafunzo hayo, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha), Bi. Sauda Msemo, alisisitiza umuhimu wa nchi za EAC kuungana na kubadilishana uzoefu katika kukabiliana  changamoto za mabadiliko ya tabianchi na masuala ya kidijitali.

"Wakati kanda inashuhudia ukuaji thabiti wa uchumi, uwiano kati ya faida za kiuchumi, hatari za mabadiliko ya tabianchi, na vitisho vya usalama wa mtandao kutokana na maendeleo ya kidijitali vinachukua nafasi kuu katika majadiliano,”  alisema kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mkurugenzi, Tawi la Benki Kuu ya Tanzania Arusha, Bi. Saphy Mahmoud.

Hatari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na ukame, mafuriko, na matukio mabaya ya hali ya hewa, yana athari kubwa katika uchumi, yakiathiri kilimo, usalama wa chakula, maisha ya watu, na miundombinu. Kozi hiyo inalenga kuzipa benki kuu katika kanda hii zana muhimu za kutekeleza kuhakikisha usalama na utulivu wa mfumo wa fedha dhidi ya changamoto hizo.

"Mafunzo haya yatatumia kanuni zinazokubalika kimataifa, ikiwa ni pamoja na mwongozo kutoka Bodi ya Utulivu wa Fedha na Kamati ya Basel ya Usimamizi wa Benki," alisema.

Kwa kutambua jukumu muhimu la kushughulikia vihatarishi vinavyohusiana na tabianchi katika kuimarisha misingi ya kiuchumi, benki kuu za EAC zinaweka kipaumbele katika kujumuisha data na habari za tabianchi katika sera zao. Mafunzo yatalenga kujenga taksonomia za mabadiliko, kusaidia masoko endelevu, na kuimarisha uwezo wa kanda katika uchambuzi wa hatari za hali ya hewa na tathmini ya uhimilivu wa hali hiyo kwa sekta ya fedha.

Katika mafunzo hayo, inatarajiwa kwamba benki kuu za EAC zitapata mijadala yenye manufaa na kuziwezesha kuweka mikakati ya kukabiliana kwa ufanisi na mabadiliko ya tabianchi na mfumo wa kidijitali wa kifedha.