Sera ya Fedha kutekelezwa kwa Riba ya Benki Kuu

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inatarajiwa kuanza kutumia mfumo wa riba katika utekelezaji wa sera ya fedha kuanzia Januari 2024. Hatua hii inalenga kudhibiti mfumuko wa bei na kuwezesha ukuaji wa uchumi kwa kuzingatia mazingira ya kiuchumi ya ndani na nje.

Akizungumza katika semina ya wahariri wa vyombo vya habari iliyofanyika  katika ukumbi wa mikutano wa BoT jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi BoT, Dkt. Suleiman Missango, amesema kuwa riba hiyo itajulikana kama Riba ya Benki Kuu na itakuwa inatokana na lengo la mfumuko wa bei na makadirio ya ukuaji wa uchumi.

“Riba ya Benki Kuu itatumika kama kigezo cha kuweka viwango vya riba kwa wateja wa benki na taasisi nyingine za fedha nchini,” alisema.

Dkt. Misssango alisema kuwa mabadiliko katika Riba ya Benki Kuu yataonyesha mwelekeo wa sera ya fedha ambapo ongezeko lake litamaanisha kupunguza ujazi wa fedha, wakati kupungua kwa riba hiyo kutamaanisha kuongeza ujazi wa fedha katika uchumi.

BoT imeweka uwiano wa 60% kwa mfumuko wa bei, 30% kwenye ukuaji wa uchumi, na 10% kwa sera ya fedha kuchangia kuweka utulivu wa kiwango cha kubadilisha shilingi dhidi ya dola ya Marekani,” alisema.

Dkt. Missango amesema kuwa mfumo huu utasaidia kuimarisha utulivu wa bei na kukuza uchumi kwa kuzingatia mabadiliko ya uchumi. Amesema kuwa mfumo wa kutumia ujazi wa fedha umekuwa ukipungua ufanisi kutokana na kasi isiyotabirika ya mzunguko wa fedha, ambayo inaweza kubadilika mara kwa mara kwa sababu ya kuongezeka kwa bidhaa mpya za huduma za kifedha na mifumo ya malipo.

“Utekelezaji wa sera ya fedha kwa kutumia riba utawezesha benki kuu kuchukua hatua za haraka na za wakati kulingana na mabadiliko ya mahitaji na upatikanaji wa fedha kwa benki za kibiashara. Hii itasaidia kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kuzingatia hali halisi ya uchumi,” amesema Dkt. Missango.

Vile vile, ameongeza kuwa mfumo huu utaongeza uwazi na uwajibikaji wa Benki Kuu katika utekelezaji wa sera ya fedha, kwani itakuwa ikitangaza maamuzi ya Kamati ya Sera ya Fedha, ikiwa ni pamoja na kiwango cha Riba ya Benki Kuu kwa umma.

Pia, amesema kuwa mfumo huu utaendana na matakwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuelekea umoja wa sarafu, kwani nchi nyingi katika EAC na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) tayari zinatekeleza mfumo huu.

Hata hivyo, Dkt. Missango amesisitiza kuwa mfumo wa kutumia riba katika utekelezaji wa sera ya fedha siyo suluhisho pekee katika kudhibiti bei na kustawisha uchumi. Ametoa wito kwa serikali na wadau wengine wa uchumi kufanya kazi kwa pamoja na benki kuu katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, uzalishaji, biashara na ajira nchini.

Naye, Meneja wa Idara wa Shughuli za Sarafu kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu BoT, Bw. Ilulu Ilulu, aliwasilisha mada kuhusu Huduma ya Upokeaji wa sarafu zisizotumika kwa muda mrefu ambapo amesema BoT inapokea sarafu za shilingi 200, 100 na 50 kutoka kwa wananchi au taasisi ili kuzibadilisha na noti.

Amesema kuwa hatua hii imechukuliwa kutokana na utafiti uliobaini kuwepo kwa sarafu nyingi ambazo hazitumiki katika mzunguko wa kiuchumi na badala yake zimetunzwa au kuwekwa nyumbani, ofisini, kwenye magari, biashara na taasisi mbalimbali nchini.

Wananchi wote wenye sarafu hizo ambazo zimetunzwa bila kutumika kwa muda mrefu na wangependa kuzibadilisha ili kupata noti au kuzitunza kama amana katika akaunti zao, wanaombwa kuziwasilisha kwenye ofisi za Benki Kuu au benki za biashara kwa ajili ya kupata huduma hiyo.