Gavana BoT,TBA Wakutana Kujadili Ustawi wa Sekta ya Benki

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, Novemba 29 2023, amekutana na Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) chini ya Mwenyekiti wake, Bw. Theobald Nsabi, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na kujadiliana, masuala mbalimbali kuhusu sekta ya benki nchini.

Katika mkutano huo uliofanyika ofisi za BoT Dar es Salaam, Gavana Tutuba amezitaka benki za biashara kuendeleza jitihada za kupunguza mikopo chechefu kwa lengo la kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha nchini.

Vilevile, Bw. Tutuba amezihimiza benki kuzingatia kanuni na miongozo mbalimbali inayosimamia fedha za kigeni ili kuimarisha soko la fedha za kigeni kwa maendeleo endelevu ya nchi.

Katika mkutano huo, Gavana amezikumbusha benki kwamba kuanzia Januari 2024, Benki Kuu itahama kutoka kutumia Mfumo wa kutayarisha Sera ya Fedha unaolenga Ujazi wa Fedha kwenda kwenye Mfumo wa Utekelezaji wa Sera ya Fedha Unaotumia Riba na kuisihi sekta hiyo kutoa ushirikiano wakati wa mabadiliko hayo.