Katika juhudi za kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni nchini, wataalamu mashuhuri wa fedha na wawakilishi kutoka Benki Kuu wamekutana katika Kongamano la Pili la Utafiti katika Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Mwanza. Semina hiyo, iliyopewa jina “Upungufu wa Dola za Kimarekani: Hatua gani bora za kuchukua,” ililenga kuchambua changamoto zinazotokana na upungufu wa dola ya Marekani katika biashara na huduma za kimataifa.
Akizungumza katika semina hiyo, Naibu Gavana, Sera za Uchumi na Fedha, Dk. Yamungu Kayandabila, alisisitiza umuhimu wa semina hiyo katika kuonyesha changamoto za kiuchumi za kimataifa na za kitaifa. Tukio hilo lililenga pia kupata maoni na mitazamo itakayosaidia kuleta utulivu wa uchumi katika kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi na uhaba wa dola nchini.
“Tunaamini kwa kufuata sera sahihi za kiuchumi, tunaweza kujenga uchumi ambao ni imara na endelevu zaidi,” alisema Dk. Kayandabila, akibainisha ustahimilivu ulioonyeshwa na uchumi wa Tanzania katika kukabiliana na misikusuko ya kiuchumi.
Dk. Kayandabila alishukuru uwepo wa wawakilishi kutoka Benki Kuu ya Ghana, Jumuiya ya Afrika Mashariki , Benki Kuu za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), washirika wa mafunzo wa Chuo cha BoT, na wajumbe kutoka taasisi za fedha na za kitaaluma, akiangazia namna ushiriki wao umewezesha kufanikiwa kwa semina hiyo.
“Ninawahimiza sisi sote kushiriki kikamilifu katika majadiliano ambayo yatakua zaidi ya fikra zilizozoeleka,” alisema Dk. Kayandabila, akisisitiza umuhimu wa fikra za ushirikiano katika kutafuta suluhisho za changamoto za kiuchumi.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha BoT na Naibu Gavana wa BoT, Bw. Julian Banzi Raphael, alisema Chuo kimeandaa semina hiyo ikiwa ni utekelezaji wa moja ya majukumu makuu ya taasisi yoyote ya mafunzo ya kufanya shughuli za utafiti kama inavyotakiwa na Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi (NACTVET).
Wasemaji wakuu wa semina hiyo walikuwa Bw. Jamhuri Ngelime, aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania, na Bw. Acevedo Sebastian, Mwakilishi Mkaazi wa IMF kwa Tanzania. Wasemaji hao walitoa maoni na mitazamo yao kuhusu sababu, matokeo, na suluhisho za mgogoro wa dola.
Semina hiyo pia ilijumuisha majadiliano ya jopo, ambapo wataalamu watano kutoka maeneo na sekta tofauti walitoa maoni na uzoefu wao kuhusu mada hiyo. Wanajopo walikuwa Bi. Getrude Machingura, Naibu Mkurugenzi kutoka Benki Kuu ya Zimbabwe; Prof. Dulacha Barako, Naibu Mkurugenzi kutoka Benki Kuu ya Kenya; Dk. Mulenga Pamu, Mshauri wa Gavana wa Benki Kuu ya Zambia; Bw. Sabasaba Moshingi, Mkurugenzi Mtendaji wa DCB; na Bw. Kennedy Komba, Mkurugenzi wa Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa jopo hilo.
Kongamano hilo ni sehemu ya mahafali ya pili ya Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania yanatarajiwa kufanyika Novemba 17, 2023 ambapo wahitimu watatunukiwa Stashahada ya Uendeshaji na Usimamizi wa Benki ya Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania na Stashahada ya Uzamili katika Uongozi wa Benki ya Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania. Mahafali hayo ni maadhimisho ya mafanikio ya kitaaluma na uthibitisho wa dhamira ya Chuo ya kukuza wataalamu wa kifedha wa siku zijazo.