Dkt. Kayandabila Azindua Fahirisi Ya Masoko Ya Fedha Ya Afrika

 

Naibu Gavana Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila, leo Novemba 15, 2023, ameongoza uzinduzi wa Fahirisi ya Masoko ya Fedha ya Afrika ya mwaka 2023 ( Africa Financial Markets Index 2023) iliyoandaliwa na benki ya Absa. Hafla hiyo imefanyika katika hoteli ya Hyatt Regency iliyopo jijini Dar Es Salaam.

Akizindua fahirisi hiyo, Dkt. Kayandabila ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi, ametaja maboresho ya mazingira ya masoko ya fedha, maendeleo katika huduma jumuishi za fedha na maboresho katika udhibiti wa masoko hayo kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia maendeleo ya masoko ya fedha nchini.

Vilevile, Dkt. Kayandabila ameipongeza benki ya Absa kwa kuandaa AFMI akisema ni nyenzo ya kuongeza uwazi na ufanisi katika masoko ya fedha

' Fahirisi ya Masoko ya Fedha imekuwa ni nyenzo muhimu katika kutathmini utendaji na fursa za maendeleo ya masoko ya fedha nchini.' alisema

Aliongeza, ''Ripoti hii inatupa uchambuzi wa kina juu utendaji wa masoko ya fedha nchini Tanzania na Afrika kiujumla, ikiainisha ubora na maeneo yanayohitaji maboresho . Ripoti hii ni kielelezo cha kazi kubwa iliyofanywa na watunga sera, mamlaka za udhibiti na washiriki wa masoko haya nchini ambao wamefanya jitihada kubwa kuhakikisha mazingira rafiki kwa ajili ya maendeleo ya masoko ya fedha"

Akizungumza Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Mkurugenzi wa Masoko ya Kimataifa wa benki hiyo, Bi. Esther Maruma, alisema, 'Tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2017, Fahirisi ya Masoko ya Fedha ya Afrika ya Absa imejitahidi kuonesha sifa za bara hili kama eneo lenye fursa na rafiki kwa uwekezaji.

"Tunafanya hivi kwa kutumia viwango vya masoko vya kimataifa kwenye masuala muhimu kama upatikanaji na uwazi wa masoko . Lengo ni kupima maendeleo katika masoko ya mitaji na kuonyesha nchi mbalimbali hatua wanazoweza kuchukua kuwavutia wawekezaji wa kimataifa kwenye masoko yao." Aliongeza- Mamlaka ya masoko la mitaji na dhamana

Kwa upande wake, Mkuu wa Utafiti wa benki ya Absa, Bw. Jeff Gable, alisema alama ya jumla ya Fahirisi ya Masoko ya Fedha ya Afrika ya Absa ya Tanzania iliongezeka mwaka huu, na nchi ilipanda nafasi mbili hadi ya 10 kwenye fahirisi.

Bw. Gable aliorodhesha maeneo ambayo Tanzania ilifanya vizuri kuwa ni uwazi wa taarifa za masoko, mazingira ya kodi na udhibiti, kina cha soko, mazingira na uwazi wa uchumi wa kati, Upatikanaji wa fedha za kigeni, uwezo wa wawekezaji wa ndani, na Viwango vya Kisheria na Utekelezaji.