Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua kitengo maalum kiitwacho Timu ya Dharura ya Kukabiliana na Changamoto za Usalama kwenye Mifumo ya Kompyuta katika Sekta ya Fedha Tanzania (TZ-FinCERT), mpango mpya utakaofuatilia, kugundua na kukabiliana na matukio yanayoathiri usalama wa mifumo ya kompyuta katika sekta ya fedha fedha nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya wadau wa TZ-FinCERT iliyofanyika kwenye ofisi ndogo za makao makuu Dar es Salaam, Novemba 14, 2023, Naibu Gavana, Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Kassim Msemo, alisema kuwa warsha hiyo inawaleta pamoja viongozi wa sekta na wataalam wa usalama wa mifumo ya kompyuta kujadili changamoto na fursa za mapinduzi ya kidijitali katika sekta ya fedha.
Alieleza kuwa jukumu kuu la TZ-FinCERT litakuwa ni kujenga uwezo wa sekta hiyo kugundua kwa wakati na kukabiliana na matukio ya usalama katika mifumo ya kompyuta. “Hii itawezesha sekta hiyo kuwa imara zaidi katika kiutambua na kudhibiti vitisho na matukio ya usalama katika mifumo ya kompyuta na kuhakikisha kuendelea kutolewa kwa huduma zinazohusiana na masuala ya fedha kwa wadau wetu,” alisema.
Alisema kuwa kuanzishwa kwa TZ-FinCERT ni hatua kubwa kuelekea kuwa na mfumo salama wa fedha nchini. Pia alisema kuwa BoT itafuatilia kwa karibu na kuchangia katika shughuli za uanzishwaji na uendeshwaji wa TZ-FinCERT kwa ufanisi,” alisisitiza.
Msemo aliongeza kuwa kiwango cha michakato ya kazi inayoendeshwa kwa mfumo katika sekta ya fedha kimekua kikiongezeka kwa kasi, lakini pia kiwango cha kufichuliwa kwa vitisho na mashambulizi katika mifumo ya kompyuta .
“Ushirikiano wa kweli kati ya serikali na wadau wasio wa serikali ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazohusiana na mtandao na kuboresha michakato ya kukabiliana na matukio ya usalama katika mifumo ya kompyuta ,” aliongeza.
Alisema kuwa kwa kujenga mfumo imara wa usalama wa mtandaoni, BoT inachangia katika lengo kuu la kitaifa la kuunda mustakabali salama wa kidijitali kwa Watanzania wote.
Waliohudhuria warsha hiyo ni wawakilishi kutoka Wizara ya Fedha, Jeshi la Polisi Tanzania, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Masoko na Mitaji Tanzania (CMSA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) , Umoja wa Watoa Huduma za Mtandao wa Simu Tanzania (TAMNOA), na Benki Kuu ya Tanzania.