Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua hatua za kuimarisha udhibiti wa utakatishaji fedha haramu kwa kusaini hati mbili za makubaliano ya ushirikiano kati ya taasisi za usimamizi na vyombo vya upelelezi.
Akizungumza katika tukio hilo lililofanyika tarehe 31 Oktoba 2023 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kudhibiti Utakasishaji Fedha Haramu, Ufadhili wa Ugaidi na Ufadhili wa Silaha za Mangamizi, Bi. Sauda Msemo, amesema kuwa hati hizo za makubaliano ni hatua muhimu katika kuimarisha udhibiti wa utakatishaji fedha haramu hapa nchini.
"Hati hizi za makubaliano zitawezesha taasisi za usimamizi na vyombo vya upelelezi kushirikiana kwa karibu katika kuzuia na kupambana na vitendo vya utakatishaji fedha haramu," alisema Bi Sauda.
Bi. Sauda alizitaka taasisi za usimamizi na vyombo vya upelelezi kutumia majukwaa yanayoanzishwa na hati hizo za makubaliano kuimarisha utendaji wao kwa kupeana taarifa, uzoefu na kuendesha mafunzo ya pamoja.
Hati ya kwanza ya Makubaliano inaanzisha mashirikiano miongoni mwa taasisi 17 za usimamizi, ikiwa ni pamoja na Benki Kuu ya Tanzania; Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu; Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana; Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania; Bodi ya Michezo ya Kubahatisha; Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni; Msajili wa Hati na Msajili wa Taasisi Zisizo za Kiserikali; Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania; Mamlaka ya Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar; Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi; Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi; Wakala wa Usajili; Ufilisi na Udhamini; Chama cha Wanasheria Tanganyika; Chama cha Wanasheria Zanzibar na Tume ya Madini. Hati hii inalenga kuziwezesha taasisi hizo kutekeleza majukumu yao ya usimamizi kwa ufanisi.
Hati ya pili ya Makubaliano inaanzisha mashirikiano miongoni mwa taasisi 13 za utekelezaji wa sheria, ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka; Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar; Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa , Usalama wa Taifa; Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar; Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Tanzania; Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar; Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai; Mamlaka ya Mapato Tanzania; Mamlaka ya Wanyama Pori Tanzania; Mamlaka ya Mbuga za Wanyama na Mamlaka ya Huduma za Misitu Tanzania. Hati hii inalenga kuziwezesha taasisi hizo kutekeleza majukumu yao ya upelelezi na uchunguzi kwa ufanisi.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kusaidia Tanzania kuboresha ufanisi wake katika kupambana na utakatishaji fedha haramu, ambao ni tatizo kubwa duniani kote.