KUBORESHA MAHUSIANO YA KIMATAIFA - GAVANA WA BoT NA MAREKANI WAKUTANA MOROCCO

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, na Gavana Lisa Cook, mjumbe wa Bodi ya Magavana wa Benki Kuu ya Marekani, wamekutana huko Marrakech, Morocco, wakati wa mikutano inayoendelea ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Kikao hicho kimetoa fursa kwa viongozi hawa wa Benki Kuu kutathmini mwenendo wa fedha na uchumi katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

Pia, wamejadiliana kwa kina kuhusu changamoto na fursa zinazokabili jumuiya ya Benki Kuu ulimwenguni, huku wakipata ufahamu wa pamoja kuhusu masuala muhimu kama vile mfumuko wa bei na sera za fedha. Viongozi hawa walipata fursa ya kubadilishana uzoefu na kujifunza kutokana na utendaji bora katika nchi zao.

Aidha, mazungumzo hayo yalizingatia pia umuhimu wa kuboresha ushirikiano kati ya Benki Kuu ya Tanzania na Benki Kuu ya Marekani. Uhusiano imara kati ya taasisi hizi mbili ni muhimu sana kwa ushirikiano wa kifedha na kiuchumi kati ya nchi hizi. Pia, wamejadili jinsi ya kuboresha ushirikiano wa kiufundi, mafunzo, na ubadilishaji wa taarifa ili kusaidia kukuza utulivu wa kifedha katika eneo la Afrika Mashariki na kimataifa.

Kikao hicho kati ya Gavana Tutuba na Gavana Cook ulikuwa hatua muhimu kuelekea kuboresha uhusiano wa kimataifa kati ya benki kuu hizi na kusaidia kukuza ustawi wa kiuchumi katika nchi zao na kanda zao. Wawakilishi hawa wa taasisi za fedha wameonyesha nia ya kushirikiana kwa karibu na kuleta mabadiliko chanya katika mifumo ya kifedha na uchumi wa dunia.