Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imehimizwa kuhusisha sera za mazingira katika utekelezaji wa majukumu yake ili kusaidia maendeleo ya shughuli za kiuchumi na ukuaji endelevu wa uchumi wa nchi.
Akizungumza alipotembelea banda la Benki kuu kwenye Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini, mkoani Geita, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Selemani Jafo, alisisitiza umuhimu wa Benki Kuu kujumuisha kipengele cha uhifadhi wa mazingira katika usimamizi wa sera ya fedha.
"Athari za mabadiliko ya tabia ya nchi ni kubwa sana. Tunapoona wilaya zingine zinakumbwa na ukame, mifugo inakufa, na mazao yanashindwa kuota, ni wakati wa kutafakari kuhusu umuhimu wa mazingira. Kama hatutalinda mazingira, uwezo wetu wa kuzalisha mazao utaathirika. Hii inaweza kusababisha upungufu wa bidhaa za kuuza nje na kufanya taifa kupoteza mapato ya fedha za kigeni," alisema.
Aidha, Dkt. Jafo aliongeza kuwa ni wajibu wa kila mdau, ikiwa ni pamoja na taasisi za kifedha kama Benki Kuu, kuchangia katika juhudi za utunzaji wa mazingira ili kuhakikisha kuwa maendeleo ya kiuchumi yanakwenda sambamba na uhifadhi wa mazingira.
Vilevile, Dkt. Jafo ameitaka BoT kuongeza juhudi katika kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa matumizi ya mifumo ya malipo katika kufanya malipo ya bidhaa na huduma mbalimbali.
Alisema kuwa mifumo ya malipo hufanya mchakato wa malipo kuwa rahisi na haraka kwakua watumiaji wanaweza kufanya malipo kwa kutumia programu za simu za mkononi au kadi za benki bila haja ya kubeba pesa taslimu au kusubiri muda mrefu katika foleni za benki au maduka.
Awali, wafanyakazi wa BoT wakiongozwa na Waziri huyo, walishiriki katika zoezi la upandaji miti kwenye viwanja vya Bombambili mkoani Geita ikiwa ni sehemu ya kuunga juhudi za serikali za utunzaji wa mazingira ili kuwezesha maendeleo ya taifa na kujenga uchumi endelevu kwa vizazi vijavyo.