MFUMUKO WA BEI MWEZI AGOSTI WABAKI PALEPALE

Kiwango cha mfumuko wa bei kwa mwezi Agosti 2023 kimebakia asilimia 3.3 kama ilivyokuwa mwezi uliotangulia. Kiwango hiki kiko ndani ya viwango vinavyokubalika kitaifa na kikanda.

Jukumu la msingi la Benki Kuu ya Tanzania ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei na kujenga mfumo wa fedha ulio imara na unaofaa kwa ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa. Hivyo, kuwa na mfumuko wa bei tulivu kunachangia Benki Kuu kutimiza jukumu lake hilo.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa, mfumuko wa bei za chakula kwa mwezi Agosti 2023 ulipungua hadi kufikia asilimia 5.6 kutoka asilimia 6.1 mwezi uliotangulia, na kutoka asilimia 7.8 katika mwezi Agosti mwaka 2022. Baadhi ya vyakula ambavyo bei zake zilishuka ni ngano na mahindi.

Hata hivyo, mfumuko wa bei unaotokana na bidhaa zisizo za chakula uliongezeka kufikia asilimia 2.4 ikilinganishwa na asilimia 2.2 mwezi Julai.

Mfumuko wa bei usiohusisha chakula na nishati uliongezeka kidogo hadi asilimia 2.2 mwezi Agosti, kutoka asilimia 2.1 mwezi uliotangulia.

Mfumuko wa bei za nishati, mafuta na huduma nyingine ulishuka hadi kufikia asilimia - 0.6 kwa mwezi huo.

Katika kipindi cha miezi 10 iliyopita, wachangiaji wakubwa kwa mfumuko wa bei ni mfumuko wa bei za chakula (kisichosindikwa) na mfumuko wa bei za bidhaa za chakula na nishati. Mchango wa nishati kwenye mfumuko wa bei ulibakia mdogo.

Wakati huo huo, viwango vya mfumuko wa bei katika kanda za EAC na SADC viliendelea kupungua kutokana na kuimarika kwa upatikanaji wa chakula. Viwango hivyo vilikuwa vinaelekea katika vile vilivyokubalika katika mtangamano.

Katika kipindi cha miezi ijayo, mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kuwa wa chini na tulivu kutokana na uwepo wa chakula cha kutosha na matarajio ya kuanza kupungua kwa bei za huduma na bidhaa duniani.

Hata hivyo, bado kuna tishio la kupanda kwa bei za mafuta kutokana na  nchi wanachama  wa OPEC+ kupunguza uzalishaji.