TANZANIA INA AKIBA YA KUTOSHA YA FEDHA ZA KIGENI

Nchi ina akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, ameeleza Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Suleiman Missango.

“Pamoja na kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa fedha za kigeni nchini, hususan dola ya Marekani, hali ya upatikanaji wa fedha za kigeni umeendelea kuwa himilivu,” ameeleza Dkt. Missango katika kikao na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam.

Amesema uhimilivu huo unatokana na kuendelea kuwepo kwa akiba ya kutosha ya fedha za kigeni nchini, ambapo hadi Jumatatu tarehe 21 Agosti 2023, akiba hiyo ilikuwa dola za Marekani milioni 5,441.

Akiba hiyo, “inatosheleza miezi 4.9 ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje. Kiasi hiki kinalingana na kipindi kabla ya changamoto ya uchumi wa dunia zilizopelekea kuwepo kwa upungufu wa fedha za kigeni,” alisema.

Aidha, mkurugenzi huyo amesema Benki Kuu inaendelea kutumia akiba iliyopo kuongeza ukwasi katika soko la fedha za kigeni nchini.

“Kuanzia mwezi Julai hadi Agosti 21 2023, Benki Kuu imeuza katika soko la fedha za kigeni dola milioni 100.5, ikilinganishwa na dola milioni 62 katika kipindi cha Julai-Septemba 2022,” ameeleza Dkt. Missango.

Amesema yangu kuangazi kwa vita ya Ukraine mwezi Machi 2022, Benki Kuu imeksiahuza katika soko la fedha za kigeni dola milioni 518.5.

Katika kikao hicho ambacho pia kiliwashirikisha wawakilishi wa mabenki na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni, Dkt. Missango amesema Serikali na Benki Kuu zinaendelea kutekeleza hatua mbalimbali kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni nchini.

“Hatua hizo ni pamoja na Benki Kuu kuongeza kiwango cha kuuza fedha za kigeni katika soko la fedha za kigeni, kuongeza vyanzo vya upatikanaji wa fedha za kigeni ikiwemo ununuzi wa dhahabu na  mikakati ya kuongeza mauzo nchi za nje na kuzalisha bidhaa mbadala wa zile zinazoagizwa nje ya nchi,” ameeleza.

Ameeleza matumaini pia kwamba uchumi wa dunia umeanza kuimarika, na hivyo kuashiria kuanza kuwepo kwa ongezeko la fedha za kigeni nchini.

Amesema ukuaji wa uchumi wa dunia unatarajiwa kufikia asilimia 3 mwaka 2023 tofauti na matarajio ya awali ya ukuaji wa asilimia 2.8. Aidha, bei za bidhaa katika soko ladunia zimeendelea kupungua, na mfumuko wa bei umeendelea kupungua katika nchi mbalimbali.

Ameeleza pia kwamba, benki kuu za nchi mbalimbali duniani, ikiwemo Marekani, zimeanza kupunguza kasi ya kuongeza riba katika kukabiliana na mfumuko wa bei.

“Mwenendo huu wa kuridhisha katika uchumi wa dunia, unaashiria kupungua kwa changamoto ya upungufu wa dola ya Marekani nchini.

Pamoja na maendeleo hayo duniani, uchuni wa Tanzania unaendelea kuimarika na kuna viashiria vya kupungua kwa changamoto za upungufu wa fedha za kigeni nchini.

Benki Kuu ya Tanzania imewataka wananchi kuondoa hofu ya upatikanaji wa fedha za kigeni.

Aidha imeviomba vyombo vya habari kutoa taarifa sahihi ili kuepusha hofu na taharuki katika upatikanaji wa fedha za kigeni nchini.

Wafanyabiashara na wananchi wametakiwa kuzingatia sheria, miongozo na kanuni za fedha za kigeni kama zilivyoanishwa katika tamko kuhusu matumizi ay fedha za kigeni nchini wa taarifa ya Benki Kuu kwa umma ya tarehe 20 Juni 2023 na kwamba fedha zitokanazo na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi kuwekwa katika mabenki hapa nchini.

Aidha, Benki Kuu imewataka wananchi kuongeza matumizi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa hapa nchini.

“Hatua hii itapunguza mahitaji ya fedha za kigeni, kuimarisha shughuli za uchumi, na kuongeza kipato kwa wananchi,” amesema Dkt. Missango na kuwataka wazalishaji kuongeza uzalishaji na unbora wa bidhaa na huduma ili kupunguza uhitaji wa bidhaa au huduma kutoka nje na kuongeza mapato ya fedha za kigeni.

Katika kikao hicho, wahariri walipata nafasi ya kuuliza maswali ambayo yalijibiwa kwa pamoja na Benki Kuu na wawakilishi wa mabenki na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni.

Upungufu wa fedha za kigeni nchini, kama ilivyo duniani kote umetokana na athari za vita kati ya Urusi na Ukraine, UVIKO-19, mabadiliko ya tabianchi, na mabadiliko ,ya mwelekeo wa sera ya fedha katika kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei duniani.