Benki Kuu ya Tanzania imefanya mkutano na benki za biashara zinazotumia mfumo wa SWIFT kufanya miamala ya fedha kutoka benki moja kwenda benki nyingine.
Mkutano huo uliofanyika leo katika kumbi za mikutano za Benki Kuu jijini Dar es Salaam, ulihusu mradi wa kuhama kutoka mfumo wa udhibiti viwango wa ISO 15022 kwenda ISO 20022.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha mada hiyo, Afisa Mwandamizi Mkuu wa Mifumo ya TEHAMA kutoka Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo ya Taifa (DNPS), Bw. Filbert Sumaye, amesema lengo la mkutano huo ni kuwaeleza wadau muendelezo wa mradi na kuboresha mifumo ya malipo ili kuweza kupitisha miamala kwa kutumia viwango vipya vya ISO 20022.
SUMAYE ameeleza kuwa faida itakayopatikana kutokana na utekelezaji wa mradi huo ni kuwezesha benki zote za biashara kupokea ujumbe wa ISO 20022 ifikapo mwezi Mei 2024.
Katika mfumo huo wadau wanaweza kuandaa ujumbe, kutuma, kupokea, kuchangia mawazo na kujibu, hivyo kupata taarifa sahihi na kwa wakati.
Aidha dunia nzima inatarajia kutumia mfumo huo wa ISO 20022 ambao utaongeza ufanisi kwa viwango vya kimataifa na kudumisha ulinzi katika vita dhidi ya utakatishaji fedha.
ISO 20022 ni kiwango cha kimataifa katika utoaji wa huduma za fedha chenye lengo la kutumia lugha mtambuka katika kubadilishana ujumbe wa fedha na takwimu.