MADUKA YA KUBADILISHA FEDHA ZA KIGENI YATAKIWA KUZINGATIA SHERIA

Wamiliki wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni wameaswa kuendesha biashara hiyo kwa kuzingatia sheria za nchi.

 

Wito huo umetolewa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ACP Jumanne Muliro, wakati wa kikao cha wafanyabiashara hao, Benki Kuu ya Tanzania na Jeshi la Polisi kilichofanyika ukumbi wa Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam. Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kujadiliana kuhusu umuhimu wa wafanyabiashara wa maduka hayo kufanya biashara zao bila kukikuka taratibu zilizowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.

 

“Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania na wafanyabiashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni.

 

“Zingatieni sheria na kanuni za fedha zinazosimamiwa na BoT ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema Kamanda Muliro.

 

Amesema Jeshi la Polisi litaendelea kushikiriana na BoT na wamiliki wa maduka ya kubadilisha fedha kuhakikisha sheria zinafuatwa na kila anayetaka kufanya biashara hiyo na kwamba watakaokiuka sheria watachukuliwa hatua za kisheria.

 

“Tumeonyesha kwa mifano jinsi ambavyo baadhi ya watu hawazingatii sheria ya kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kuwa wanafungua maduka majumbani kwao, wapo wanaofanya biashara hii katika maeneo yasiyo rasmi kama stendi za mabasi, bodaboda na vituo vya taxi, ambao hawajasajiliwa na kufuata sheria na kanuni za biashara hii,” alieleza.

 

Ili kuepusha madhara kwa mtu binafsi na hata taifa kutokana na biashara isiyo rasmi, Kamanda Muliro alisema Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na taasisi mbali mbali za serikali na zisizo za kiserikali kuhakikisha sheria zinazoongoza shughuli mbali mbali za biashara hiyo zinafuatwa.

 

Akiwasilisha mada kuhusu sheria na kanuni za biashara ya kubadilisha fedha za kigeni katika kikao hicho, Meneja Msaidizi kutoka Idara ya Taasisi Maalum za Fedha kutoka BoT, Bw. Omar Msuya, alisema sheria ya fedha za kigeni ikikiukwa mhusika anaweza kupigwa fani na kufungwa.

 

“BoT inaendelea na ukaguzi katika katika maeneo mbali mbali nchini, ili kuhakikisha kwamba  sheria na kanuni hazikiukwi,” alisema.

 

Bw. Msuya alisema kwa mujibu wa kanuni za BoT zinazohusu usimamizi wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni za 2019, zinamtaka kila anayetaka kufanya biashara hiyo kuwa na leseni, na zinakataza kufanya biashara  ya kubadilisha fedha za kigeni bila leseni.

 

Wakizungumza katika kikao hicho, wamiliki wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni wamewataka Watanzania kuendelea kulinda thamani ya shilingi ya Tanzania kwa kutuma Shilingi ya Tanzania wanapofanya manunuzi.