Mfumo wa Sera ya Fedha

SERA YA FEDHA
Sera ya Fedha ina jukumu la kuhakikisha ujazi wa fedha katika uchumi wa nchi unawiana na malengo ya utulivu wa bei na ukuaji wa uchumi. Kamati ya Sera ya Fedha ya Bodi ya Wakurugenzi ambayo huongozwa na Gavana ndiyo yenye majukumu ya kuandaa sera ya fedha kila baada ya miezi miwili kwa mujibu wa Tamko la Sera ya Fedha..

MFUMO WA SERA YA FEDHA WA BENKI KUU YA TANZANIA
Mfumo wa Sera ya Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania umelenga kuhakikisha uwepo utulivu wa bei kwa kudhibiti ujazi wa fedha. Mfumo wa Sera ya Fedha ya Fedha unajumuisha masuala yafuatayo:

Lengo la Sera ya Fedha
Lengo la msingi la Sera ya Fedha  ni kuhakikisha uwepo wa  utulivu wa bei, yaani mfumuko mdogo wa bei ulio stahilimivu usiozidi asilimia 5 katika kipindi cha  muda wa kati. Lengo hili linaendana  na vigezo vya muunganiko wa uchumi mpana vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambavyo ni asilimia 8 na asilimia 3-7 kwa mtiririko huo. Lengo la utulivu wa bei  ni muhimu ili kuwa na ukuaji endelevu wa uchumi nchini. Ili kufikia lengo hilo Benki Kuu ya Tanzania inahakikisha kuna kiwango sahihi cha ukwasi katika uchumi na utulivu wa riba na  thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na sarafu za nchi nyingine.

Lengo la kati
Benki Kuu inadhibiti mfumuko wa bei  kwa kudhibiti ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana (M3). Ujazi wa fedha kwa tafsiri pana unajumuisha fedha zilizo kwenye mzunguko nje ya mfumo wa benki (currency in circulation) na amana  za wakazi wa Tanzania katika Benki za biashara, zikiwemo amana za fedha za kigeni.

Lengo la uendeshaji
Ili kudhibiti ujazi wa fedha, Benki Kuu hudhibiti pesa taslimu (reserve money) inayojumuisha fedha zilizo nje ya mfumo wa kibenki, fedha zilizo kwenye mabenki ya biashara na fedha zilizo kwenye akaunti za benki za biashara zilizopo Benki Kuu.

Nyenzo za Sera ya Fedha
Benki Kuu ya Tanzania hutumia nyenzo mbalimbali  kutekeleza Sera ya Fedha  ambazo ni uuzaji na ununuzi wa  dhamana (debt securities), uuzaji na ununuzi wa fedha za kigeni  kutoka soko la  fedha za kigeni baina ya mabenki, nyenzo za repo and reverse repo, mikopo kwa mabenki ya biashara na kiasi cha amana za benki  za biashara kinachotakiwa kuwa Benki Kuu (Statutory Minimum Reserve) na huduma za muda mfupi za ukwasi kwa mabenki (intraday and Lombard loan facilities).

Uwasilishaji wa Sera ya Fedha kwa umma
Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikihakikisha uwazi katika uundaji na utekelezaji wa Sera ya Fedha. Maamuzi ya Kamati ya Sera ya Fedha (Monetary Policy Committee) kuhusu sera ya fedha iliyoamuliwa huwasilishwa kwenye mkutano na wakuu  wa benki za biashara na pia huwasilishwa kwa umma kupitia vyombo vya habari. Vilevile, Benki Kuu huchapisha ripoti za vipindi mabalimbali zinazoonesha sera ya fedha iliyopo, utekelezaji wake na muelekeo wa uchumi wa Tanzania kwa ujumla. Ripoti hizo huwekwa pia kwenye tovuti ya Benki Kuu.