Matokeo ya Utekelezaji wa Sera ya Fedha
Mtiririko wa sera ya fedha unaainisha namna utekelezaji wa sera ya fedha unavyochagiza shughuli za kiuchumi na kudhibiti mfumuko wa bei. Kwa kawaida matokeo ya utekelezaji wa sera ya fedha huchukua miezi kadhaa kuanza kuonekana katika shughuli za uzalishaji pamoja na bei za bidhaa na huduma nchini. Kwa muktadha huo, sera ya fedha hulenga kudhibiti vichocheo vya mfumuko wa bei katika kipindi kijacho (forward looking) kwa kuangalia maoteo na mwelekeo wa viashiria mbalimbali vya kiuchumi.
Maamuzi ya Sera ya Fedha
Kamati ya Sera ya Fedha ya Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu ya Tanzania (Monetary Policy Committee) ndiyo yenye jukumu ya kuamua na kupanga riba ya sera ya fedha (riba ya Benki Kuu) kwa kila robo ya mwaka, kuendana na malengo mapana ya kiuchumi yaliyoainishwa kwenye Tamko la Sera ya Fedha. Kila mwanzo wa mwaka, Benki Kuu huandaa na kuanisha mwelekeo sera ya fedha kupitia Tamko la Sera ya Fedha. Tamko hili huidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu na kuwasilishwa bungeni kupitia kwa Waziri wa Fedha.
Uratibu wa Sera ya Fedha
Uandaaji na utekelezaji wa sera ya fedha hulenga pia kuoanisha malengo yake na sera nyingine za kiuchumi hususan sera ya kibajeti, ili kuondoa mkanganyiko wa malengo katika sera hizi. Hii ni kwa sababu sera ya kibajeti ina mchango mkubwa katika kufanikisha au kuathiri malengo ya sera ya fedha. Kwa kuzingatia muingiliano huo, kamati mbalimbali za sera za fedha zimeundwa ili kuzingatia suala hili. Mbali na kamati ya sera ya fedha, pia kuna kamati ya pamoja ya kufanya makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kila mwezi. Kamati hii ya pamoja huongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na huudhuriwa na wajumbe mbalimbali ikiwemo wajumbe kutoka Benki Kuu.
Wigo wa Sera ya Fedha
Benki Kuu ya Tanzania huandaa na kutekeleza Sera ya Fedha ikiwa kwa lengo la kuhakikisha utulivu wa bei nchini ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuhakikisha uimara wa sekta ya fedha. Hata hiyo ni vyema ikafahamika kuwa, kwa wakati mwingine, mfumuko wa bei wa jumla huathiriwa na mitikisiko ya upande wa ugavi (supply side shocks) ambazo ni nje ya wigo wa sera ya fedha. Vilevile, sera ya fedha ya kuongeza ukwasi kwa muda mfupi ndiyo inayoweza kuchochea ukuaji wa uchumi kutokana na kutobadilika kwa bei za bidhaa (perceived rigidity of prices). Hivyo, utekelezaji wa sera ya fedha ya kuongeza ukwasi kwa kipindi kirefu hausababishi kuongezeka kwa ukuaji wa uchumi isipokuwa hupelekea kuongezeka kwa bei za bidhaa.