Historia ya Benki Kuu

Benki Kuu ya Tanzania ilianza kazi rasmi tarehe 14 Juni 1966. Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho na kuwezesha kutungwa kwa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 1978 na Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 1995. Kwa sasa, Benki Kuu ya Tanzania inaendesha shughuli zake kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006.

Kabla ya kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania, historia ya masuala ya noti na sarafu nchini imegawanyika katika sehemu mbili: kabla ya kuanzishwa kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (EACB) mwezi Desemba 1919; na baada ya kuanzishwa kwa bodi hiyo hadi mwezi Juni 1966 ilipoanzishwa Benki Kuu ya Tanzania.

Masuala ya noti na sarafu kabla ya mwaka 1919 yalikuwa yanaendeshwa tofauti upande wa Tanganyika na wa Zanzibar. Katika kipindi hicho, Tanganyika ilikuwa chini ya utawala wa Kijerumani, wakati Zanzibar ilikuwa na serikali yake (ya Waarabu). Sarafu iliyokuwa inatumika Tanganyika ni Rupia ya Kijerumani, ambayo ilitengenezwa kwa fedha, pamoja na sarafu nyingine iliyoitwa Heller ambayo ilikuwa moja ya mia ya Rupia. Fedha iliyokuwa ikitumika Zanzibar ni Rupia ya India. Pia, magamba (shells) na ng’ombe vilitumika katika kuhifadhi thamani na wakati mwingine kama fedha kwa ajili ya kununua na kuuza bidhaa na huduma.

Shughuli za kibenki hapa nchini zilianza mwaka 1905 wakati Benki ya Deutsch-Ostafrikanische ilipofungua ofisi yake Dar es Salaam. Benki hiyo ilipewa kibali na Serikali ya Ujerumani kuchapisha noti na kutengeneza sarafu kwa ajili ya matumiz nchinii. Kiwanda cha muda cha kutengeneza sarafu kilianzishwa Tabora. Mwaka 1911, benki nyingine ya Kijerumani iliyoitwa Handelsbank fuer Ostafrika ilifungua tawi lake Tanga.

Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Tanganyika iliwekwa chini ya usimamizi wa Uingereza na kuanza kutumia mfumo wa fedha uliokuwa unatumika Kenya na Uganda:

(a) Kwa kuanzisha Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (EACB) mwezi Desemba 1919, na
(b) Kwa kupiga mnada mali za benki za Kijerumani na kuruhusu benki za Kiingereza kufungua ofisi zake Tanganyika.

Kanuni za kikatiba, kazi na mamlaka ya bodi ya sarafu zilieleza kwamba EACB iliundwa ili kusimamia usambazaji wa noti na sarafu katika eneo lililokuwa chini ya utawala wa Waingereza katika Afrika Mashariki pamoja na maeneo mengine tegemezi katika ukanda huo, ambayo yangeweza kuongezwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza (Secretary of State), ili kuhakikisha kwamba kuna kiwango cha kutosha cha noti na sarafu.

Mwanzoni, EACB ilifanya kazi Tanganyika, Kenya na Uganda. Zanzibar ilijiunga na EACB mwaka 1936. Nchi zilizokuwa chini ya ukoloni zilijiunga na kujitoa katika bodi hiyo baada ya muda mfupi.

EACB ilikuwa na mamlaka ya kuchapisha noti na kutengeneza sarafu zake baada kuidhinishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, kwa ajili ya kusambazwa katika maeneo iliyokuwa inayahudumia. Kiwango cha kubadilisha fedha za EACB na paundi ya Uingereza kilipangwa na Waziri wa Mambo ya Nje. Thamani ya sarafu ya EACB ilikuwa inalindwa na paundi ya Uingereza. EACB ilihitimisha kazi zake mwaka 1966 wakati nchi za Tanzania, Kenya na Uganda zilipoamua kuanzisha benki kuu zao.

Kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania

Kufuatia uamuzi wa kuivunja Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na kuanzishwa kwa Benki Kuu katika kila nchi za Tanzania, Kenya na Uganda; Bunge la Tanzania lilipitisha Sheria ya Benki Kuu Na. 12 ya mwaka 1965.

Benki Kuu ya Tanzania ilianza kazi rasmi tarehe 14 Juni 1966. Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho na kuwezesha kutungwa kwa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 1978 na Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 1995. Kwa sasa, Benki Kuu ya Tanzania inaendesha shughuli zake kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006.