Sarafu

Usimamizi wa Sarafu
Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 inatoa mamlaka kwa Benki Kuu pekee kutengeneza na kutoa fedha (noti na sarafu) kwa matumizi nchini Tanzania. Hiyo ndiyo fedha halali kwa ajili ya malipo nchini Tanzania. Hivyo, Benki Kuu ina wajibu wa kubuni na kuagiza noti na sarafu ili kukidhi mahitaji ya fedha nchini. Fedha ya Tanzania ni Shilingi, ambayo imegawanywa kwenye senti 100. Benki Kuu inahakikisha kwamba sarafu yake ni ubora unaokubalika kwa sarafu nzuri ambao ni;
  • Kukubalika na umma kama fedha kwa ajili ya kufanya malipo ya bidhaa na huduma;
  • Alama za usalama ambazo zinafanya iwe vigumu kutengeneza noti na sarafu zisizo halali;
  • Uwezo wa sarafu kudumu kwa muda mrefu.
Soma zaidi..

Noti na sarafu zilizotolewa na Benki Kuu ya Tanzania
Tangu ilipoanzishwa mwaka 1966, Benki Kuu ya Tanzania imetoa matoleo mbalimbali ya noti na sarafu kama kiunganishi hiki kinavyoonesha Soma zaidi..

Haki na wajibu wa mteja wa benki katika kufanya miamala
Kuhakikisha wateja wa benki za biashara wanapata aina ya noti na sarafu wanazotaka na kuhakikisha wanatunza fedha hizo vizuri na kwa usalama, benki zote za biashara zinatakiwa kuwakumbusha wateja wao haki na wajibu kama ulivyoelezwa kwa kifupi katika kiambatanisho hiki ( Haki na Wajibu wa Wateja za Benki katika Kufanya Miamala). Hii itasaidia kuwa na noti na sarafu safu katika mzunguko an hivyo kupunguza gharama za kutengeneza noti na sarafu.

Noti na Sarafu za Kumbukumbu (numismatics)
Benki Kuu ya Tanzania hutoa Noti na Sarafu maalum kwa ajli ya kumbukumbu za matukio muhimu ya kitaifa. Sarafu hizi huuzwa au kutolewa kama zawadi wakati wa matukio hayo. Pia, sarafu za kumbukumbu zinahitajika sana na watu wanaokusanya sarafu. Mifano ya Sarafu za Kumbukumbu zimeonyeshwa katika kiunganishi hiki (Commemorative Coins).

Historia ya Sarafu Tanzania

Wageni wa kwanza kufika nchi za Afrika Mashariki, hasa Tanzania, walikuwa ni Wareno waliofika katika karne ya 15 na Waarabu katika karne ya 17. Wakati huo hakukuwa na fedha kama njia ya ubadilishanaji wa bidhaa na huduma, hivyo biashara zilifanyika kwa kubadilishana vitu kwa vitu (Barter Trade).


Kabla ya mwaka 1919, mifumo wa fedha wa Tanganyika iliyokuwa chini ya utawala wa Ujerumani, na Zanzibar iliyokuwa na serikali yake, ilikuwa tofauti. Tanganyika ilitumia Rupee ya Kijerumani kwa ajili ubadilishanaji wa bidhaa na huduma wakati Zanzibar ilitumia Rupia za madini ya fedha (silver rupees).
Mnamo mwaka 1905, Wajerumani walianzisha benki ya Biashara (Deutsch-Ostafrikanische Bank) jijini Dar es Salaam. Benki hii ilikuwa na kiwanda cha kutengeneza pesa ya kijerumani pale Tabora ambapo kiwanda hiki kiliwajibika kutengeneza pesa za kutosha mahitaji ya fedha kwa uchumi.


Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Tanganyika iliwekwa chini ya uangalizi wa Uingereza na mfumo wake wa sarafu ukaunganishwa na ule wa Kenya na Uganda ambazo zilikuwa chini ukoloni wa Waingereza. Rasilimali zote za mabenki ya KIjerumani zilipigwa mnada ili kuruhusu Benki za Uingereza kufungua ofisi zao. Fedha aina ya 'Specie' na 'Pice' ikaanzishwa kwa ajili ya kutumika bara. Mwaka 1905 sarafu ya Rupia ya India ilifanywa kuwa sarafu rasmi ya nchi za Afrika Mashariki hadi ilipoanzishwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki.


Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (the East African Currency Board (EACB)) ilianzishwa ili kusimamia masuala ya fedha kwa nchi zilizokuwa chini ya utawala wa Uingereza kuanzia 1919 hadi mwaka 1965. Bodi hii ilianzishwa mara tu baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, yaani Waingereza walipoanza kuitawala Tanganyika. Wajibu wa Bodi hii ulikuwa ni kusimamia usambazaji wa fedha katika Afrika Mashariki, kuhakikisha kuna kiwango cha fedha kinachohitajika katika mzunguko ili kukidhi mahitaji. Bodi hii ilianza na nchi za Tanganyika, Kenya na Uganda. Zanzibar ilijiunga mwaka 1936.Bodi ilikuwa na madaraka ya kutoa noti na sarafu kulingana baada ya michoro ya zitakavyokuwa kupitishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza. Waziri huyo aliweka kiwango cha kubadilisha fedha kati ya sarafu ya Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na poundi ya Uingereza. Kazi kubwa ya Bodi ilikuwa ni kuhakikisha kwamba thamani ya shilingi katika nchi za Afrika Mashariki inakuwa sawa na shilingi ya UIngereza; hili liliwezekana kwa sababu dhamana za poundi ya Uingereza zilitumika kuipa uzito sarafu ya Afrika Mashariki muda wote wa uhai wake. Ilipofika mwaka 1923, shilingi iliimarika na kuwa sarafu rasmi kwa nchi za Kenya, Uganda na Tanganyika.
Bodi hii ilivunjika mwaka 1966 baada ya nchi za Afrika Mashariki za Tanzania, Kenya na Uganda kupata uhuru na kila moja kuamua kuanzisha Benki Kuu yake.