Bodi ya Wakurugenzi ni chombo chenye madaraka na mamlaka ya juu kinachotoa maamuzi ya kisera katika muundo wa Benki Kuu ya Tanzania. Kwa mujibu wa kifungu cha nane (8) cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, Bodi ya Wakurugenzi ina wajibu wa kuamua sera za Benki Kuu, kuidhinisha bajeti na mgawanyo wa faida inayotokana na shughuli zake.
Bodi ina wajumbe 10. Wanne ni wakurugenzi watendaji wanaoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; wajumbe wawili wanaoingia kutokana na nyadhifa zao na wengine wanne wanateuliwa na Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katibu wa Benki Kuu pia ni mjumbe anayeingia kwa wadhifa wake mwenye wajibu wa kutoa huduma za Sekretarieti.
Muundo wa Bodi ya Benki Kuu ni kama ifuatavyo:
Majukumu ya Bodi Katika kufanya kazi zake; Bodi ya Wakurugenzi inasaidiwa na Kamati nne, mbili miongoni mwao zimeundwa kisheria. Kamati hizo mbili ni Kamati ya Sera ya Fedha na Kamati ya Ukaguzi. Bodi ya wakurugenzi inayo mamlaka ya kuunda kamati zingine kadiri inavyoona inafaa. Zaidi ya kamati zilizoundwa kisheria, Bodi imekasimu baadhi ya majukumu yake kwa kamati nyingine mbili, ambazo ni Kamati ya Usimamizi wa Shughuli za Benki na Kamati ya Fedha na Uwekezaji.
Kamati ya Sera ya Fedha Kamati hii inasaidia Bodi ya Wakurugenzi katika kupitia malengo ya sera ya fedha, kupitia ripoti za utafiti na mabadiliko muhimu ya Sera ya Uchumi na Fedha kabla ya kupitishwa na Bodi. Mamlaka na Madaraka ya Kamati pia yanahusu kupitia muelekeo wa mapato na matumizi ya Serikali, kupitia shughuli za usimamizi wa madeni na ripoti za kisheria za Benki Kuu zinazohusiana na utekelezaji wa Sera ya Fedha . Aidha, kamati hii inaainisha mwelekeo wa sera ya fedha kwa muda wa miezi miwili inayofuata. Muundo wa Kamati hii umebainishwa katika kifungu cha 12(1) cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006. Kamati hii inawajumuisha Gavana wa Benki kama mwenyekiti, Manaibu Gavana na wakurugenzi wawili wasiokuwa watendaji. Mikutano ya kamati inafanyika kila baada ya miezi miwili.
Kamati ya Ukaguzi Kamati ya Ukaguzi inaundwa kwa mujibu wa kifungu cha 12(1) cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 ina wajumbe wengi wasiokuwa wakurugenzi watendaji. Kamati hii inaongozwa na Mkurugenzi asiyekuwa Mtendaji wa Benki Kuu. Naibu Gavana –Utawala na Udhibiti wa Ndani ndiye mtendaji pekee wa Benki Kuu katika Kamati hii.
Kamati ya Usimamizi wa Mabenki Kamati hii ina wajibu wa kusimamia udhibiti wa ndani na mifumo kwenye mabenki na taasisi za fedha; kitengo cha usimamizi wa shughuli za Benki, utoshelevu wa muundo wa sheria na usimamizi uliopo; utendaji wa shughuli za mabenki, taasisi za fedha na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni (bureau de change) kwa lengo la kuhakikisha usalama na uimara katika mfumo wa shughuli za kibenki. Aidha, kamati hii inapitia ripoti za uthabiti wa fedha kabla ya kuchapishwa na masuala ya usimamizi kwa ujumla.Muundo wa Kamati hii uko kwenye ridhaa ya Bodi. Wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Shughuli za Benki ni pamoja na Gavana wa Benki ambaye ni Mwenyekiti, Manaibu Gavana, Mwakilishi wa Wizara ya Fedha (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania), Katibu Mkuu wa Hazina, Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Wakurugenzi wawili wasiokuwa watendaji.
Kamati ya Fedha na Uwekezaji Kamati ya Fedha na Uwekezaji ina wajibu wa kupitia bajeti zilizopendekezwa, upangaji upya wa kasma/mafungu ya fedha na maombi ya bajeti ya nyongeza; ripoti za utendaji wa bajeti kila robo mwaka; Kanuni za Fedha na Sheria ndogo ndogo za wafanyakazi na Mpango Mkakati wa Mwaka wa Shirika. Kamati hii pia inapitia sera za fedha na sera nyingine za ndani na marekebisho yanayohusiana nazo. Aidha, inapitia usahihi wa sera ya uwekezaji ya Benki na Mkakati wa upangaji wa rasilimali. Kamati hii pia inasimamia muundo wa Usimamizi wa Matukio ya Dharura na Muundo wa Usimamizi wa Miradi. Wajumbe wa Kamati hii ni pamoja na Gavana wa Benki ambaye ni Mwenyekiti, Manaibu Gavana na Wajumbe Watatu wa Bodi wasio watendaji.
Menejimenti ya Benki Kuu (Management) Menejimenti ya Benki Kuu inaundwa na Gavana, Manaibu Gavana, Wakurugenzi, Mameneja na Mameneja Wasaidizi. Gavana na Manaibu Gavana huteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania kwa mujibu wa Kifungu cha 8 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, na hutumikia nyadhifa hizo kwa muda wa miaka mitano. Aidha, huweza kuteuliwa tena kutumikia nyadhifa hizo kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Wakurugenzi, Mameneja na Mameneja Wasaidizi huteuliwa na Gavana kwa kuzingatia vigezo vya utendaji bora. Gavana ni Mtendaji Mkuu wa Benki Kuu na pia ni mwenyekiti wa Bodi ambaye anawajibika katika maamuzi yote ya kisera yanayotolewa na Bodi. Vilevile, Gavana anawajibika katika Menejimenti kuteua au kumuachisha kazi mfanyakazi kutokana na sababu mbalimbali na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Sn. | Picha | Jina | Nafasi |
---|---|---|---|
1. | Bw. Emmanuel M. Tutuba | Gavana | |
2. | Bw. Julian Banzi Raphael | Naibu Gavana, Utawala na Udhibiti wa Ndani | |
3. | Dkt. Yamungu M. Kayandabila | Naibu Gavana, Uchumi na Sera | |
4. | Bi. Sauda Kassim Msemo | Naibu Gavana, Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha | |
5. | Dkt. Juma M. Akil | Katibu Mkuu Hazina (SMZ) | |
6. | Bw. Elijah G . Mwandumbya | Representative from the Ministry of Finance - URT | |
7. | Bi. Esther J. Manyesha | Mkurugenzi | |
8. | Bw. Ngosha S. Magonya | Mkurugenzi | |
9. | Prof. Esther K. Ishengoma | Mkurugenzi | |
10. | Bw. Nassor S. Ameir | Mkurugenzi | |
11. | Bw. Palloty M. Luena | Secretary to the Board | |
Sn. | Picha | Jina | Nafasi |