Mbinu na Nyenzo za Usimamizi

Mfumo wa Usimamizi unaozingatia Vihatarishi (Majanga) ni mfumo wa usimamizi  unaotumiwa na Benki Kuu ya Tanzania katika kusimamia benki an taasisi za fedha zenye leseni kufanya kazi nchini. Chini ya mfumo huo wa usimamizi, mkazo ni katika maeneo ambayo uwezekano mkubwa wa vihatarishi kutokea katika kila benki au taasisi ya fedha ili kuhakikisha kuna ufanisi katika usimamizi. Mwelekeo huo unaiwezesha Benki Kuu ya Tanzania kuweka kipaumbele katika kutenga fedha kulingana na madaraja ya uwezekano wa vihatarishi/majanga kwa kila benki na taasisi ya fedha na kufuatilia ufanisi wa njia za kutambua, kupima, kufuatilia, kuzuia kwa kiwango cha chini aina sita ya vihatarishi/majanga.

Benki Kuu ya Tanzania inatumia njia mbili za ukaguzi na ufuatiliaji ambazo ni ukaguzi wa moja kwa moja wa nyaraka mbalimbali katika benki au taasisi ya fedha husika na uchamguzi wa taarifa mbalimbali zinazowasilishwa Benki Kuu na benki au taasisi za fedha. Benki Kuu inafanya ukaguzi ili kujua utendaji wa kila benki au taasisi ya fedha kutokana na taarifa nyingi zinazopokelewa kutoka katika taasisi hizo kila siku, kila wiki, kila wiki mbili, kila mwezi, kila miezi mitatu, kila nusu mwaka na kila mwaka au kupitia taarifa za muda mfupi za maombi ya kufanya ukaguzi wa moja kwa moja. Madhumuni ya kupitia uthabiti wa benki na hali yake ya biashara ni kupunguza uwezekano wa benki kufanya maamuzi yanayoweza kusababisha vihatarishi/majanga na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo mbalimbali ya uendeshaji mzuri wa biashara ya benki yanayotolewa mara kwa mara na Benki Kuu.

Benki Kuu hutumia nyenzo zifuatavyo katika kutekeleza kikamilifu usimamizi wa benki na taasisi za fedha: -

Ukaguzi wa Moja kwa Moja

Ukaguzi wa moja wa moja unahusu kutembelea benki au taasisi ya fedha husika ili kukagua maeneo yote au maeneo yanayolengwa kukaguliwa, hasa yanayolenga angalau maeneo sita ya vihatarishi/majanga ya  mikopo, ukwasi, masoko, uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu, kimkakati na uendeshaji.

Taratibu za ukaguzi zinalenga kuwa na nyaraka za kutosha kuweza kuchunguza uwezo wa kutambua, kupima, kufuatilia na kudhibiti vihatarishi/majanga. Katika kufanya ukaguzi wa jumla, Benki Kuu inafuatilia kubaini kama vihatarishi/majanga katika benki au taasisi ya fedha husika huibuliwa na kudhibitiwa ipasavyo.. Ukaguzi huo wa msingi unahusu taratibu za kupitia maeneo yafuatayo; Ubora wa Mali na Vihatarishi vya Mikopo; Ukwasi na Vihatarishi vya Ukwasi; Vihatarishi vya Masoko; Vihatarishi vya Utendaji, Vihatarishi vya Kimkakati, Vihatarishi vya uzingatiaji sheria, kanuni na taratibu, Ukaguzi na Udhibiti wa Ndani, Utoshelevu wa Mtaji, Uongozi/Menejimenti na Mapato.

Pia, Benki Kuu hutumia mfumo wa upimaji unaoangalia Utoshelevu wa Mtaji, Ubora wa Mali, Ubora wa Menejimenti, uwezo wa Mapato, Ukwasi na uwezekano wa kuathirika na Vihatarishi vya Masoko (CAMELS) katika kuchambua uwezo wa kifedha ufanisi wa uendeshaji wa taasisi. Chini ya uchambuzi kwa kutumia CAMELS, benki na taasisi zote za fedha zinapimwa kwa njia ya usawa na usimamizi wa karibu unazilenga benki na taasisi za fedha ambazo zinaonyesha udhaifu wa kifedha na uendeshaji and hali isiyoridhisha.

Upembuzi wa viashiria mbalimbali huzingatia ukubwa wa taasisi, aina na ukubwa wa shughuli zake na nafasi yake kipimo cha vihatarishi.. Aidha, Benki Kuu inachambua uimara wa mifumo ya usimamizi wa ndani wa taasisi husika.

Mfumo wa Uchambuzi wa Taarifa Zinazowasilishwa Benki Kuu na Taasisi za Fedha

Uchambuzi wa uthabiti kifedha wa benki na taasisi za fedha hufanywa kwa kupitia takwimu na taarifa zingine zinazowasilishwa na benki na taasisi fedha kielektroniki kila siku, kila wiki, kila baada ya wiki mbili, kila mwezi, kila robo mwaka, kila nusu mwaka na kila mwaka au  zinazowasilisha katika vipindi vifupi kama kuna mahitaji ya kufanya hivyo. Kutokana na uchambuzi Taarifa ya Onyo la Mapema hutayarishwa na huiwezesha Benki Kuu kufanya maamuzi sahihi kuhusu uthabiti wa sekta ya fedha katika ngazi ya taasisi moja na kwa ujumla.

Katika kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha uthabiti na usalama wa sekta ya fedha, Benki Kuu ya Tanzania hutumia nyenzo zifuatazo: -

  1. Mikutano iliyopangwa na menejimenti za benki na taasisi ili kujadiliana kuhusu utendaji, hali ya vihatarishi na mikakati na masuala mengine yoyote ya usimamizi ambayo yanaweza kuathiri usalama na uthabiti wa benki au taasisi ya fedha;
  2. Mikutano ya dharura na menejimenti za benki na taasisi za fedha kwa ajili ya kujadiliana kuhusu maendeleo ya biashara au mipango inayoibuka kutokana na mchakato wa usimamizi wa vihatarishi au uchambuzi wa nyaraka mbalimbali.
  3. Mikutano na wakaguzi wan je wa benki na taasisi za fedha kujadiliana kuhusu masuala ya usimamizi, na
  4. Mawasiliano na wasimamizi wengine.